Rwanda Yamkosoa Vikali Jenerali Muhoozi Kwa Kauli Za Kikabila

Serikali ya Rwanda imekemea vikali kauli za kikabila zilizotolewa na Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, katika mfululizo wa ujumbe wa mtandaoni uliomhusisha mfanyabiashara Odrek Rwabwogo na Rais Paul Kagame.

Rwanda Yamkosoa Jenerali Muhoozi Kwa Kauli Za Kikabila

Msemaji wa serikali, Yolande Makolo, alisema Rwanda haitakubali kurudishwa nyuma kwa mijadala ya kikabila ambayo imekuwa chanzo cha maafa makubwa nchini.

“Tumetumia miaka 32 kujenga mshikamano baada ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi. Hatutaki na hatuhitaji siasa za kikabila,” alisema.

Makolo alisisitiza kuwa maoni kuhusu Rwanda yanaweza kutolewa, lakini hayapaswi kupotosha wananchi au kuhusisha taifa na fikra za kikabila. Aliongeza kuwa mizozo ya ndani ya Uganda inapaswa kubaki ya Uganda na isiingize Rwanda.

Kauli hizo zilitolewa wakati Muhoozi akiendelea na mgogoro wa hadhara na Rwabwogo, ambapo alitilia shaka asili ya kikabila ya mfanyabiashara huyo na baadaye kumtaja Rais Kagame kama “Mututsi hatari zaidi.”

“Nina mashaka kama kweli Odrek ni Muhima. Hata mienendo yake haionekani hivyo, huenda akawa Muhutu.” aliandika Muhoozi  na kuongeza kuwa “Mututsi hatari zaidi niliyewahi kukutana naye maishani ni Rais Kagame. Akicheka kupita kiasi, ujue tayari hatima yako imekwisha”

Rwanda imesema maneno hayo ni ya uchochezi na yanapingana na dhamira ya kitaifa ya mshikamano.

Wakati Muhoozi akiendelea kumshutumu Rwabwogo kwa madai ya ufisadi ambayo hayajathibitishwa mahakamani, Kigali imeweka wazi kuwa haitavumilia majaribio ya kufufua siasa za kikabila ambazo zilitumbukiza taifa katika janga la mwaka 1994.