Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, ameiambia Mahakama kuwa kampeni ya “Tone Tone” iliyoanzishwa na chama hicho imekusanya Shilingi milioni 302 hadi sasa.

Mnyika ametoa kauli hiyo Septemba 1, 2026, wakati akiendelea kutoa ushahidi wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, huku akijibu maswali kutoka kwa mawakili wa Serikali.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Kathbert Mbilinyi, Mnyika amekiri kuwa CHADEMA imekuwa ikiendesha kampeni ya “Tone Tone”, akisema fedha zinazopatikana kupitia kampeni hiyo zinaelekezwa kwenye maeneo maalum, ikiwemo kusaidia kupunguza ukali wa maisha kwa watendaji wa chama.
Mbilinyi amemhoji Mnyika kuhusu utaratibu wa ulipaji wa posho kwa viongozi na watendaji wa chama, huku Mnyika akisema Katibu Mkuu pamoja na Sekretarieti yake bado wanadai posho.
Mnyika amesema hali hiyo inatokana kwa kiasi kikubwa na chama hicho kuzuiwa kufanya shughuli za kisiasa kwa siku takribani siku 309 pamoja na kukosa ruzuku.
Katika sehemu nyingine ya ushahidi wake, Mnyika amekanusha kufahamu taarifa za mwanachama wa CHADEMA aliyewahi kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu madai ya mipango ya chama, mifumo maalum ya mawasiliano na mipango ya kusimamia vurugu siku ya uchaguzi.
Pia amesema alifahamu kupitia vyombo vya habari kuwa baadhi ya watu walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa ya uhaini baada ya uchaguzi, lakini akasema hafahamu madai kwamba watuhumiwa hao waliwaambia polisi kuwa walifanya vurugu hizo kwa maelekezo ya Tundu Lissu.
Haya ni baadhi ya maswali na majibu yaliyojiri mahakamani:
Katuga: Unajua au hujui kesi ya jinai sio mapenzi bali ni ushahidi?
Mnyika: Najua.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kuwa Katibu Mkuu kama wewe ni mhusika wa kujua idadi ya wanachama wa Chadema?
Mnyika: Sihusiki moja kwa moja, ni wasaidizi chini yangu ndio wanaofanya kazi hizo.
Katuga: Unaposema wasaidizi chini yako maana yake wanafanya kazi za Katibu Mkuu?
Mnyika: Za Katibu Mkuu.
Katuga: Uliwahi kufuatilia malalamiko ya WanaChadema mtandaoni?
Mnyika: Hapana, malalamiko gani?
Katuga: Unafahamu au hufahamu kuhusiana na mwanachama aliyeita waandishi wa habari na yeye kuelezea kile kilichopangwa na chama na kile kilichotokea wakati wa uchaguzi?
Mnyika: Sifahamu.
Katuga: Unafahamu kwamba mwanachama huyo aliuambia umma kwamba mipango ile ilipangwa na chama na kuratibiwa?
Mnyika: Sifahamu.
Katuga: Unafahamu mwanachadema huyu kwenye taarifa yake alisema kwamba kulikuwa na mifumo maalum ya simu ili kuwasiliana kupata taarifa ili kufanikisha mpango huo?
Mnyika: Sifahamu.
Katuga: Unafahamu kwenye taarifa ya mwanachama huyo kwamba kulikuwa na mipango ya kusimamia vurugu siku ya uchaguzi?
Mnyika: Sifahamu.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama uliwahi kujitokeza kumpinga huyu mwanachadema anayeitwa Shengoma wa Chadema kwamba matukio ya Oktoba mlihusika?
Mnyika: Simfahamu.
Katuga: Unafahamu ama hufahamu baada ya uchaguzi na zile zilizowendelea baada ya uchaguzi kuna watu walikamatwa?
Mnyika: Walikamatwa wakaachiwa kwa maelekezo ya Rais.
Katuga: Iambie Mahakama kwamba hao watu waliokamatwa walifikishwa mahakamani kwa makosa ya Uhaini?
Mnyika: Niliona kwenye vyombo vya habari.
Katuga: Unafahamu au hufahamu kwamba washtakiwa katika mahojiano yao polisi walieleza kwamba hizo fujo walizifanya kutokana na maelekezo ya Tundu Lissu?
Mnyika: Sifahamu.
Katuga: Ukiwa kama Katibu wa Chama uliwahi kwa njia yoyote kufanya mahojiano na mtu ambaye alikuwa na kesi za Uhaini?
Mnyika: Sifahamu.
Katuga: Umetuambia sana masuala ya Demokrasia, hebu tuambie maana yake ni nini?
Mnyika: Ni utawala unaoundwa na watu kwa ajili ya watu.
Wakili wa Serikali Kathbert Mbilinyi
Mbilinyi: Ni kweli chama chako kimekuwa kikiendesha kampeni ya Tone Tone?
Mnyika: Ni kweli.
Mbilinyi: Ni kweli kwamba mpaka sasa mmetoa takwimu ya kiasi kilichopatikana?
Mnyika: Ndiyo.
Mbilinyi: Mpaka sasa mmekusanya kiasi gani?
Mnyika: Milioni 302.
Mbilinyi: Chadema inalipa watendaji wake posho?
Mnyika: Ndiyo.
Mbilinyi: Mara ya mwisho mmewalipa watendaji wenu lini?
Mnyika: Mwezi uliopita.
Mbilinyi: Na kwa mfano unatokea ushahidi kwamba hujawalipa posho watendaji wako toka mwaka jana, nani atakuwa mkweli?
Mnyika: Wote tutakuwa wakweli, kwa sababu chama kilizuiwa kufanya siasa siku 309 lakini pia kilizuiwa kupata ruzuku.
Mbilinyi: Hebu ieleze Mahakama kwamba viongozi wakuu wa Chadema wako wangapi?
Mnyika: Mwenyekiti Tundu Lissu, John Heche, Makamu Mwenyekiti Zanzibar Said Mzee Saidi, Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Bara Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Ally Ibrahimu Juma.
Mbilinyi: Ukiachana na Mwenyekiti, wewe shahidi, na Makamu Mwenyekiti Bara, hao wengine waliobaki wanadai posho?
Mnyika: Katibu Mkuu na Sekretarieti yake bado inadai posho, kwa hiyo nipo kwenye orodha ya wanaodai.
Mbilinyi: Hebu ieleze Mahakama kwa nini msitumie kulipa posho watendaji wakuu au hata wewe mwenyewe?
Mnyika: Tone Tone ipo kwa ajili ya malengo ya kupunguza ukali wa maisha ya watendaji lakini pia inaenda maeneo mahususi.
Mbilinyi: Hizo posho ambazo mnalipa watu mahususi mnalipa kupitia akaunti zao au?
Mnyika: Kupitia akaunti zao.
Lissu ambaye mbali na kuwa mwanasiasa lakini ni Wakili wa Mahakama Kuu, anakabiliwa na kesi ya uhaini akidaiwa kutenda kosa la kuitishia Serikali, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC) Rekebu ya mwaka 2023.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kutamka na kuandika (kuchapisha) mtandaoni maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Maneno hayo yanayodaiwa kuwa ya uhaini, Lissu alitamka kuwa : “Wanasema kitu kimoja hapa, msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Shahidi huyo bado anaendelea na ushahidi wake kwa upande wa Jamhuri kwa kuhojiwa maswali ya dodoso