Huku wapenzi wa muziki mtindo wa rhumba wakisubiri kumuona Koffi Olomide akitumbuiza kwenye jukwaa la Kigali Arena mnamo Disemba 4, baadhi ya watu wakiongozwa na wanaharakati wa jinsia wanataka mwanamuziki huyo wa rhumba apigwe marufuku kutumbuiza mjini humo kutokana na sifa yake ya kuwadhalilisha wanawake.
Mwimbaji huyo maarufu amewahi kuhusishwa na madai ya kuhusika katika vitendo vya udhalilisaji wa wanawake mnaomo mwaka 2016 na kufukuzwa nchini Kenya baada ya kumpiga teke mmoja wa wacheza densi wake katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta nchini humo.
Alishtakiwa kwa tuhuma kama hizo na mamlaka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka wa 2016 kwa kumpiga teke mmoja wa wacheza densi wake.
Koffi Olomide pia ana kesi mahakamani nchini Zambia, ambako alizuiwa kuingia baada ya kumpiga mwandishi wa habari mjini Lusaka mwaka wa 2012.
Mnamo mwaka wa 2019, Koffi alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na mahakama nchini Ufaransa baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji dhidi ya mmoja wa wachezaji wake wa zamani alipokuwa na umri wa miaka 15. Tabia yake ya jeuri mara nyingi imekuwa ikiwazuia waandalizi wa hafla kumwalika kutumbuiza kwenye matamasha yao lakini haionekani kuwa hivyo Rwanda baada ya waandaji kuthibitisha onyesho lake mjini Kigali mnamo Desemba 4 katika ukumbi wa Kigali Arena.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Intore Entertainment, Bruce Intore inayoandaa tamasha hiyo amesifiwa kwa jukumu kubwa la kurejesha tamasha na burudani mjini Kigali baada ya miezi 18 ya marufuku zilizowekwa kutokana na athari za UVIKO 19.
Hata hivyo, baadhi ya wapenzi wa muziki walikosoa chaguo lake la kumleta Kigali mwanamuziki ambaye sifa yake imekuwa ikihusishwa na kesi za ubakaji na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wasichana.
Mwanaharakati mashuhuri wa jinsia nchini Rwanda Juliet Karitanyi alidai kuwa itakuwa makosa kumkaribisha mwanamuziki mwenye sifa kama hiyo katika nchi ambayo haivumilii vitendo vyovyote vinavyohusiana na unyanyasaji wa kijinsia.
“Koffi Olomide ni mnyanyasaji anayejulikana, alipigwa marufuku nchini Kenya mwaka wa 2016, baada ya kumpiga mchezaji wake mmoja katika uwanja wa ndege wa Nairobi … hakuna vile mtu huyu atakavotumbuiza Kigali, ni aibu kwa nchi yetu … kati ya hayo, unamkaribisha Koffi Olomide wakati wa Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia?” alidai Karitanyi kwenye akaunti yake ya Twitter.
Uwezekano wa mwimbaji huyo kutumbuiza katika tamasha hilo wikendi ijayo haijulikani huku maombi ya kumwekea marufuku ikongezeka.
“Kwa kumkubali mtu huyu kutumbuiza Kigali, tunawadhalilisha wahasiriwa hawa; tunakubali kuwachukulia kama si kitu na, kama nchi, tunakubali kutowajibika. PIGA MARUFUKU TAMASHA HILI,” Karitanyi aliomba.
Maombi hayo yamewaeweka shinikizo kwa waandaaji wa hafla hiyo ambao walidhani mwanamuziki huyo ndiye chaguo bora la kuanza msimu wa sherehe kutokana na muziki wake ambao kwa miaka mingi umependwa nchini Rwanda.