Shirika la kitamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO siku ya Jumanne liliongeza densi ya rumba ya Congo kwenye orodha yake ya urithi wa kitamaduni, na kuzua shangwe katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchini Congo-Brazzaville.
Mkutano wa UNESCO uliidhinisha maombi ya pamoja ya nchi hizo mbili ya kuongeza rumba kwenye orodha yake ya Turathi za Utamaduni za Binadamu Usioonekana. Densi ya rumba itakuwa inaorodheshwa pamoja na rumba ya Cuba, muziki wa aina ya pygmy wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na ngoma za Burundi.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi alipokea habari hiyo kwa furaha huku raia kutoka mataifa yote mawili wakionyesha furaha yao kwenye mitandao ya kijamii.
“Rumba ni utambulisho wetu! Kutambuliwa kwake kimataifa ni fahari na hazina kwetu.” alisema waziri wa utamaduni wa DRC Catherine Furaha.
Wataalamu wamegundua asili ya rumba katika ufalme wa zamani wa Afrika ya kati wa Congo, ambapo watu walicheza ngoma iliyojulikana kama “Nkumba.”
Neno hili linamaanisha kitovu kwani densi hiyo inahusisha mwanamume na mwanamke wakicheza kwa karibu.
Waafrika walileta muziki na utamaduni wao hadi Amerika wakati wa biashara ya utumwa. Mitindo ya muziki ya densi uliibua mtindo wa jazz uliopo Amerika kaskazini kwa sasa.
Rumba imetambulishwa na historia ya kisiasa ya mataifa hayo mawili ya Congo kabla na baada ya uhuru na “ipo katika nyanja zote za maisha ya kitaifa” Andre Yoka Lye, mkurugenzi katika taasisi ya kitaifa ya sanaa ya DRC katika mji mkuu Kinshasa, aliiambia AFP.
“Hazina hizi kutoka Congo na ambazo zimesafirishwa kote duniani ni sehemu ya fahari yetu,” msemaji wa serikali ya DRC Patrick Muyaya aliandika kwenye Twitter wiki iliyopita.
Nyota wa Rumba mara kwa mara hujipata kwenye utata na kashfa.
Mahakama ya Ufaransa siku ya Jumatatu ilimtia hatiani mwimbaji mashuhuri wa DRC Koffi Olomide kwa kuwashikilia wacheza densi wake wanne wa zamani kinyume na matakwa yao wakati wa ziara zake.
Lakini raia wa nchi zote mbili wanasema ngoma hiyo inaendelea na wanatumai kuongezwa kwake kwenye orodha ya UNESCO kutaipa umaarufu mkubwa hata miongoni mwa Wakongo.
“Ni jukumu letu la pamoja kukuza rumba,” alisema waziri wa mawasiliano wa DRC Muyaya.