Wanafunzi nchini Uganda hatimaye wamerudi shule leo Jumatatu 10 Januari baada ya miaka miwili kukaa majumbani.
Mamilioni ya wanafunzi wanarudi darasani karibu miaka miwili baada ya kusimamishwa kwa masomo kwa sababu ya janga la UVIKO 19.
Wanafunzi wapatao milioni 15 hawajahudhuria shule nchini Uganda tangu Machi 2020.
“Shule zote zimetekeleza miongozo na taratibu ili kuhakikisha watoto wanarudi salama shuleni, na hatua zimewekwa kuhakikisha wale ambao hawatatii wanafanya hivyo,” Waziri wa Elimu John Muyingo aliiambia AFP.
Muyingo amesema shule zozote za kibinafsi zitakazo dai karo ya juu zitachukuliwa hatua.
Harakati za kuwarudisha watoto shuleni zilisababisha msongamano wa magari katika mji mkuu Kampala.
Mashirika ya kutetea haki za watoto yamekosoa uamuzi wa Uganda wa kufunga shule kwa muda wa wiki 83, muda mrefu zaidi kuliko nchi nyingine yoyote duniani.
“Ni lazima shule ziwe wazi kwa kila mtoto, kila mahali,” shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za watoto UNICEF lilisema kwenye Twitter.Shirika la Save the Children lilisema wanafunzi huenda wakatatizika na masomo yao baada ya kuwa nyumbani kwa muda mrefu, na kuonya kuwa kunaweza kuwa na viwango vya juu vya wanafunzi kuacha shule katika wiki zijazo iwapo mikaktati madhubuti haitawekwa.
Uganda imerekodi visa 153,762 vya UVIKO-19 na vifo 3,339, kulingana na takwimu za hivi punde za serikali zilizotolewa Januari 7.