Dodoma yapitiwa na tetemeko la ardhi

Tetemeko hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana limetajwa kuwa na ukubwa wa 5.5 katika kipimo cha richter

0

Taasisi ya Jeolojia na Utafiti wa Madini (GST) imesema tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.5 katika kipimo cha richter limetokea mkoani Dodoma na kusababisha taharuki na sintofahamu kwa wakazi wa mkoa huo.

 Mjeolojia Mwandamizi wa taasisi hiyo Gabriel Mbogoni amesema tetemeko hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 7 usiku, kitovu chake kilikuwa Kaskazini Mashariki mwa mji wa Dodoma kwenye safu za milima ya Chenene.

Amesema kitovu cha tetemeko hilo ni umbali wa kilometa 44 kutoka Dodoma Mjini na lina ukubwa wa 5.5 katika kipimo cha richter.

“Hadi sasa hivi (mchana) hatujapata taarifa yoyote ya kutokea madhara zaidi ya taharuki na watu kuzusha sintofahamu kwa wakazi wa Dodoma,”amesema.

Kwa mujibu wa Mjeolojia huyo  hadi kufikia leo mchana taarifa walizozipata za mahali ambako tetemeko hilo limeyakumba maeneo ya mkoa wa Dodoma hasa katika maeneo yanayozunguka mji wa Dodoma, ukubwa wa tetemeko unaweza kusababisha nyufa katika majengo huku akibainisha kuwa madhara yanayoweza kusababishwa na ukubwa wa tetemeko yanategemea uimara wa majengo.

Mbogoni amesema Dodoma ipo katika ukanda wa bonde la ufa la Afrika Mashariki, eneo ambalo ni tete kwa matetemeko ya ardhi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted