Wanadiplomasia wakuu wa Amerika walikutana na wanaharakati wanaounga mkono kuwepo kwa uongozi wa demokrasia Jumatano nchini Sudan kwa mazungumzo ya kujadili njia ya kusonga mbele baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana, ubalozi wa Washington mjini Khartoum ulisema.
Sudan imetikiswa na maandamano ya mara kwa mara na ukandamizaji wa haki za watu tangu unyakuzi wa kijeshi wa Oktoba 25 ulioongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan. Mapinduzi hayo yilivunja serikali na kuyumbisha mchakato wa mpito uliostahili kurudisha utawala wa kiraia.
Maandamano ya kupinga mapinduzi yamekabiliwa na vikosi vya usalama ambavyo hadi sasa vimesababisha vifo vya watu 71 — wengi wao wakipigwa risasi– na mamia kujeruhiwa, kulingana na madaktari.
Takriban waandamanaji saba waliuawa siku ya Jumatatu pekee, madaktari walisema, katika moja ya siku ambappo kulishuhudiwa umwagaji mkubwa wa damu za waandamanaji wanaopinga mapinduzi.
Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika Molly Phee na mjumbe maalum wa Pembe ya Afrika, David Satterfield, walifanya mikutano na familia zilizopoteza jamaa zao waliouawa wakati wa maandamano, ubalozi wa Amerika ulisema.
Pia walikutana na wanachama wa Chama cha Wanataaluma wa Sudan (SPA), mwavuli wa vyama vya wafanyakazi ambavyo vilichangia sana maandamano ambayo yalimuondoa madarakani rais Omar al-Bashir mwezi Aprili 2019. SPA pia imetoa wito wa maandamano ya kupinga mapinduzi.
Wanadiplomasia hao wameratibiwa kukutana na wengine wakiwemo viongozi wa kijeshi na viongozi wa kisiasa.
“Ujumbe wao utakuwa wazi:Amerika imejitolea kuhakikisha kuwa uhuru, amani na haki inapatikana kwa watu wa Sudan,” Wizara ya Mambo ya Nje ya Amerika ilisema kabla ya ziara hiyo.
Wanadiplomasia hao walifanya mazungumzo ya awali nchini Saudi Arabia na “Marafiki wa Sudan” – ikiwa ni kundi la nchi za Magharibi na mataiya ya Kiarabu yanayopendekeza kurejeshwa kwa kwa utawala wa kiraia.
Katika taarifa yake, kundi hilo liliunga mkono mpango wa Umoja wa Mataifa uliotangazwa wiki iliyopita wa kufanya mashauriano ya ndani ya Sudan ili kuuvunja mzozo huo wa kisiasa.
“Tunawaomba wote kushiriki kwa nia njema na kurejesha imani ya umma katika mchakato kuelekea kupatikana kwa uongozi wa kidemokrasia,” kikundi hicho kilisema.
Wakati wanadiplomasia wa Amerika walikuwa wangali nchini Sudan, Burhan alitangaza kwamba makamu wa mawaziri — ambao baadhi yao walihudumu kabla ya mapinduzi na baadhi walioteuliwa baadae – sasa watakuwa mawaziri.
Taarifa kutoka ofisi yake imeliita hili “baraza la mawaziri linalosimamia masuala ya nchi”.
Lakini halina waziri mkuu, kwani waziri mkuu wa kiraia Abdalla Hamdok alijiuzulu mapema Januari baada ya kujaribu kushirikiana na jeshi.
Tangu Jumanne, maduka mengi yalifungwa na barabara zilifungwa mjini Khartoum kama sehemu ya kampeni ya uasi wa raia kupinga mauaji ya hivi punde ya waandamanaji.
Waendesha mashtaka, maprofesa wa vyuo vikuu, na madaktari walijiunga na maandamano hayo.
Mamlaka ya Sudan mara kwa mara imekanusha kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji, na kusisitiza kuwa maafisa wengi wa usalama wamejeruhiwa wakati wa maandamano. Jenerali wa polisi aliuawa kwa kuchomwa kisu wiki jana.