Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam kesho inatarajia kuanza kusikiliza shauri la kikatiba la kupinga kujiuzulu kwa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai na mchakato wa kumpata Spika mpya kwa kile kilichodaiwa kuwa utaratibu ulikuwa ni batili
Uamuzi huo uliotolewa na Mahakama hiyo jana mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji John Mugeta.
Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, mdaiwa namba moja ni Job Ndugai, wa pili ni Bunge na wa tatu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mdaiwa wa pili na watatu wanawakilishwa na Mawakili Wakuu wa Serikali, Mussa Mbura, Deodatus Nyoni, Andrew Chang’a na Wakili wa Serikali, Stanley Kalokola.
Sababu iliyoifanya Mahakama kutoa uamuzi huo ni kutokana na kwamba Shauri hilo lilitakiwa kuanza kusikilizwa jana, lakini Ndugai hakuwapo wala wakili wake.
Wakili wa Serikali Mkuu, Mussa Mbura alidai shauri lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa, lakini mdaiwa wa kwanza Ndugai hakuwapo na upande wa serikali haukuandaa majibu ya kiapo kinzani kwa sababu walipata taarifa jioni.
Wakili Mussa aliiomba Mahakama wapewe siku 14 ili wajibu na kwamba tukio la kujiuzulu Spika lilitokea Januari 6, mwaka huu na kesi ilifunguliwa Januari 21, walalamikaji Mbatia walipata muda wa siku 14 kuandaa kesi na hawaoni kama kuna dharura.
Wakili Mpare Mpoki akijibu hoja hiyo, alidai kuwa dharura ipo kwa sababu kuna uchaguzi wa Spika wanauwahi, akichaguliwa mwingine kutakuwa na maspika wawili.
“Tunachoharakia uchaguzi wa Spika usifanyike, busara ya mahakama hii inatakiwa itoke kabla ya uchaguzi wa spika Januari 31, mwaka huu.Mahakama pekee ndiyo inayoweza kusimamisha uchaguzi wa Spika, hati ya wito waliyopewa serikali ilikuwa kesi inasikilizwa (leo) jana, hivyo walipaswa kuandaa majibu ya kiapo,“ alidai Mpoki.
Mahakama ilizingatia hoja na umuhimu wa suala lililoko mbele yake, ikaagiza mjibu maombi wa kwanza Ndugai apelekewe hati ya wito mkononi sio kwa email kama ilivyofanyika, kabla ya leo saa 8.30 mchana, majibu upande wa serikali yafike muda huo.
Jaji Mugeta aliahirisha shauri hilo hadi kesho kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Mbatia anapinga utaratibu uliotumiwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu na mchakato wa kupata spika mwingine.Kesi hiyo ya kikatiba namba mbili ya mwaka 2022 ilifunguliwa chini ya hati ya dharura na inasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu.
“Katiba imeweka utaratibu, Spika akitaka kujiuzulu anatakiwa kwenda kufanya hivyo kwa watu waliomchagua ambao ni wabunge.Utaratibu uliotumiwa na Ndugai ni batili haukubaliki kikatiba,” alisema Mbatia.
Katika kesi hiyo Mbatia anawakilishwa na jopo la mawakili 10 akiwamo Wakili Mpare Mpoki na Jeremiah Mtobesya.
Job Ndugai alijiuzulu uspika Januari 6, mwaka huu na Januari 21 mwaka huu, Dk. Tulia Ackson aliteuliwa kugombea nafasi hiyo.