Amuua mjamzito kisa deni la gunia mbili za mahindi

Mtuhumiwa adai alifanya hivyo baada ya kuona halipwi deni lake kila anapoenda kudai

0

Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia  Philipo Vincent (22), kwa tuhuma za kumuua kwa kumkata mapanga mjamzito na watoto wake wawili

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Theopista Mallya, alisema kuwa polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo kwa kuwa alijaribu kujinyonga ndipo walimkamata, na walipomuhoji alisema kuwa anataka kujiua kwa kuwa hana amani baada ya kufanya mauaji hayo.

Mallya alisema walipomuhoji zaidi, alikiri kufanya mauaji hayo kwa kuwa alikuwa amemkopesha mjamzito huyo  gunia mbili za mahindi na alipomdai alionekana kufanya ukaidi wa kumlipa. 

Alisema kuwa mtuhumiwa huyo alipokuwa akienda kwa mwanamke huyo kudai fedha kiasi cha shilingi 100,000 kama fidia ya gunia hizo za mahindi,  alimjibu kuwa asimdai kwa nguvu kwa kuwa hakumlazimisha amkopeshe, kauli iliyomuudhi mtuhumiwa na kuamua kufanya mauaji hayo.

“Mtuhumiwa huyo alinunua panga jipya na kulinoa vizuri, na siku ya Januari 14 usiku alikwenda nyumbani kwa marehemu na kisha kufanya mauaji hayo na kutokomea,” alisema Mallya.

Mallya ameongeza kuwa  polisi walipomuhoji sababu za kuwaua na watoto, alijibu kuwa aliamua kuwachinja kwa kuwa watoto hao walimuona wakati anamuua mama yao na pia wanamfahamu kwa kuwa amekuwa akienda katika nyumba hiyo mara kwa mara kudai fedha, hivyo wangemtaja.

Mapema wiki hii, jeshi hilo lilitoa taarifa kuhusu tukio hilo likisema kuwa tukio hilo linadhaniwa kutokea usiku wakati mama huyo na watoto wake wakiwa ndani ya nyumba yao, kisha watu waliotekeleza mauaji hayo kuingia ndani.

Mallya alisema mume wa mwanamke huyo ambaye yuko Dar es Salaam, alianza kumtafuta mkewe kwa kumpigia simu, lakini ilikuwa inaita bila kupokelewa.

Alisema alipopiga kwa muda mrefu simu hiyo ilizima, hali inayoonyesha kuwa ilizima kwa kuishiwa chaji na kila alipojitahidi kupiga haikupatikana.

Baada ya hapo alimpigia rafiki yake, Paul Leonard, na kumwagiza aende akaione familia yake na alifika nyumbani hapo saa 2:30 usiku na alishangaa kukuta mlango umefungwa nje kwa kufuli, hivyo aliamua kuwaita viongozi wa kijiji na walipofika na kubomoa mlango na kuingia ndani walikuta mwanamke huyo aliyekuwa na ujauzito wa miezi minane akiwa amechinjwa pamoja na watoto wake Milliam (8) na William (4).

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted