Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
TRC yasaini mkataba wa ununuzi wa behewa 1430 kwa ajili ya SGR - Mwanzo TV

TRC yasaini mkataba wa ununuzi wa behewa 1430 kwa ajili ya SGR

Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa (kushoto), pamoja na  Kaimu Meneja wa Kampuni ya CRRC International Tang Yun Reng (kushoto) wakisaini mkataba wa ununuzi wa Behewa 1430 za mizigo kati ya Shirika la Reli Tanzania na Kampuni ya CRRC International kutoka nchini China unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 127.2.

Waziri wa ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame mbarawa ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa ununuzi wa Behewa 1430 za mizigo kati ya Shirika la Reli Tanzania na Kampuni ya CRRC International kutoka nchini China unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 127.2 kwa ajili ya reli ya kisasa SGR.

Imeelezwa kuwa mkataba huo ni wa ununuzi wa Behewa 1430 za mizigo za reli ya kisasa – SGR ambao, ni wa miezi 12 sawa na mwaka mmoja utakaohusisha usanifu na utengenezaji wa Behewa kwa ajili ya kubeba mizigo ya aina mbalimbali kulingana na aina ya behewa na matakwa ya mteja kupitia reli ya kisasa.

Waziri wa ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame mbarawa amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha huduma ya usafiri wa mizigo inaimarika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa lengo la kuongeza pato la taifa na kukuza uchumi.

“Ujenzi wa Reli ya kisasa unaoendelea hivi sasa kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro ambacho kimefika 95%, Morogoro – Makutupora ambacho kimefika 81% na kipande cha Mwanza – Isaka ambacho kimefika 4% ni ishara tosha kwamba Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuongeza ufanisi na kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji kupitia reli” amesema Waziri Prof Mbarawa.

Aidha,Profesa Mbarawa amesema kutokana na uwezo mkubwa wa reli ya kisasa Behewa hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mrundikano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam ambapo treni moja itakuwa na uwezo wa kubeba Tani 10,000 kwa mkupuo ambayo ni sawa na malori 500.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa amezitaja aina za Behewa zitakazonunuliwa kupitia mkataba huo kuwa ni pamoja na Behewa 600 aina CCB kwa ajili ya kubeba makasha, Behewa 400 aina ya CLB  ili kubeba mizigo ya jumla ikiwemo Sukari, Saruji, Chumvi, Pamba, Tumbaku na Kahawa, Behewa 190 aina ya PTB kubeba mafuta aina zote,na Behewa 70 aina ya HLB kwaajili ya Mabomba, Mbao, Magogo na Vyuma, Behewa 50 aina ya MGB kwaajili ya kubeba magari na Behewa 50 aina ya CWB (Cattle Wagon Bogie) kwaajili ya kubeba Ng’ombe.

Mkataba huu ni miongoni wa mikataba kadhaa ambayo TRC imesaini kwa ajili ya manunuzi ya vichwa na behewa za abiria na mizigo kwaajili ya shughuli za uendeshaji wa reli ya kisasa. 

TRC ilisaini Mkataba na Kampuni ya EUROWAGON ya Uturuki tarehe 1 Oktoba, 2020 kwa ajili ya ununuzi wa vichwa viwili (2) vya treni ya umeme na behewa 30 za abiria. Mkataba huu una thamani ya EURO milioni 26.60, ambapo mkandarasi anatarajiwa kuleta vifaa hivyo mwezi Aprili, 2022.

Kadogosa amesema kitaalamu ili kuzalisha faida katika biashara ya usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kisasa itahitaji angalau kusafirisha mizigo kwa umbali usiopungua KM 500, hivyo wanatarajia kwamba kukamilika kwa manunuzi na kuwasili kwa behewa hizo mapema mwaka Februari 2023, kutakwenda sambamba na kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa Morogoro – Makutupora ambapo kwa umbali huo huduma ya usafirishaji mizigo itaweza kuleta tija kwa taifa.