Serikali ya Tanzania imeyafungulia magazeti manne yaliyofungiwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa
Uamuzi huo umetangazwa leo na Waziri wa Habari na Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari, nchini humo Nape Nnauye wakati akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Nape amesema, “Leo hapa nitatoa leseni ya magazeti yaliyofungiwa ya MwanaHALISI, Mawio, Tanzania Daima na Mseto, kifungo kimetosha. Kikubwa kazi iendelee.”
Waziri huyo amewaomba waandishi wa habari kuaminiana katika utendaji kazi kwani yeye pia ni mwanahabari mwenzao.
“mimi ni mwandishi wa habari mwenzenu. Hiki ninachokieleza ndicho kipo kwenye moyo wa Rais Samia na uelekeo wa serikali ya awamu ya sita, tufanye kazi pamoja.”
Akizungumza kwa niaba ya magazeti yaliyopewa leseni, Mkurugenzi wa Kampuni ya Halihalisi Limited wachapishaji wa gazeti la MwanaHALISI ndugu Saidi Kubenea amesema, “nikushukuru sana kwa hatua kubwa kwa kufungua ukurasa mpya kwa kutupa leseni.”
Kubenea ambaye pia ni mwandishi wa habari amesema, ni muhimu sana viongozi kusikiliza, wananchi wao kwani hakuna aliyekamilika, huku akiahidi kuwa watafanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya uanahabari
Magazeti hayo yalimaliza adhabu miaka miwili iliyopita lakini pamoja na kumaliza adhabu hiyo bado hayakupewa leseni yake na licha ya kuwa walikwenda mahakamani na kushinda kesi
“Magazeti haya yalimaliza adhabu miaka miwili nyuma na bado yalishinda kesi mahakamani lakini hayakurudi mtaani, tunamshukuru sana Rais Samia kwani bila yeye bila shaka yasingerudi,” amesema Kubenea
Aidha Waziri Nape ameiagiza Idara ya Habari Maelezo kwa kushirikiana na wahariri na taasisi zingine za habari ndani ya muda mfupi kuandaa kikao cha wadau wa habari kuzungumza marekebisho yaliyopelekwa Serikalini ya sheria ya habari.
“Kwenye hicho kikao mwisho wake tutatengeneza kamati ndogo ambayo itatokana na waandishi wa habari tushauriane tupitie kifungu hadi kifungu tuone ni namna gani wapi tunakubaliana halafu tupeleke marekebisho bungeni ya kupitia upya sheria ya habari”
Nape Nauye ambaye aliteuliwa na Rais Samia kuongoza wizara hiyo January 8,2022, amewataka waandishi wa habari kuweka tofauti zao za nyuma kuhusu sheria ya habari kwani wakati huo yeye pia akiwa Waziri wa Habari mambo hayakuwa kama hivi sasa.
“Mimi nikiwa Waziri nakumbuka nilisimamia sheria ile, mazingira ya wakati ule tofauti na sasa, kwahiyo tutaipitia tutakubaliana yatakayowezekana kubadilika tutabadilisha kwasababu ni maaagizo ya Rais. Haya mazungumzo hayafanyi sheria isimame baadhi ya mambo lazima yaendelee, yale yenye utata lazima tuyape muda mfano lile la elimu lilikuwa na utata basi tuongeze mwaka mmoja wakati tunaendelea na mazungumzo,” amesema.