Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Ushahidi wa shahidi mahususi Kesi ya Mbowe wakosekana - Mwanzo TV

Ushahidi wa shahidi mahususi Kesi ya Mbowe wakosekana

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA akiwa kwenye gari ya mahabusu akirudishwa gerezani

Kwa sasa ni muda na siku tu  ndio inangojewa kwa hamu na ghamu kuhusu hatma ya mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi yenye makosa ya Ugaidi ndani yake.

Hatua hiyo ni baada ya Jamhuri kuieleza Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joachim Tiganga, anayesikiliza kesi hiyo kwamba haitapeleka mashahidi zaidi, hivyo kuomba kufunga ushahidi.

Mahakama sasa itatoa uamuzi siku ya Ijumaa, Februari 18 majira ya saa 8 mchana iwapo Mbowe na washtakiwa wengine wana kesi ya kujibu au la. 

Wakati shauri hilo linaanza takribani miezi mitano iliyopita, Upande wa Jamhuri, walidai kuwa watakuwa na mashahidi 24 na vielelezo 19 katika kuijenga kesi hiyo, lakini hadi jana ambapo walifunga ushahidi wao  walikuwa wamepeleka mashahidi 13 tu, swali ni je 11 wako wapi?, wamegoma kutoa ushahidi au? Swali hilo hadi sasa ndilo linaloendelea kuulizwa mitandaoni.

Itakumbukwa kuwa mlalamikaji katika kesi hiyo, ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz, ambaye amestaafu na ndiye ambaye shahidi mahususi katika kesi hiyo lakini hatapanda kizimbani kutoa ushahidi.

Kamishna Boaz ni mlalamikaji katika kesi hiyo na ndiye aliyedaiwa kupewa taarifa na Luteni Dennis Urio kwamba Mbowe amemtuma atafute makomandoo waliostaafu au kufukuzwa jeshini ili ashirikiane nao kufanya vitendo vya kigaidi katika mikoa ya Morogoro, Moshi, Arusha,  Mbeya na Mwanza.

Luteni Urio ni shahidi wa 12 katika kesi hiyo ambaye alitoa ushahidi huo mbele ya jaji Joachim Tiganga.

Pia Urio alimwambia DCI Robert Boaz kwamba Mbowe na wenzake wana mpango wa kuwadhuru viongozi wa serikali akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Ikumbukwe pia karibu mashahidi wote wa upande wa Jamhuri waliofika mahakamani kutoa ushahidi walikuwa wanamtaja DCI Robert Boaz kwamba ndiye aliyewapa maagizo kuhusu kesi hii.

Sasa Kwanini Robert Boaz hatoi ushahidi?.

Kitendawili cha kesi hii kitateguliwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi siku hiyo ya Ijumaa.

Mashahidi wa Jamhuri waliowahi kufika kutoa ushahidi katika kesi hiyo ni Luteni Denis Urio, Justine Kaaya, aliyekuwa msaidizi wa Lengai Ole Sabaya, akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro. Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, ACP Ramadhan Kingai. Inspekta Mahita Omary Mahita.

Wengine ni Mrakibu wa Polisi, Jumanne Malangahe, Inspekta Goodluck Minja, Inspekta Tumaini Swila na Inspekta Innocent Ndowo.

Freeman Mbowe alikamatwa jijini Mwanza akiwa anajiandaa kuhudhuria kongamano la Katiba lilillokuwa limeandaliwa na chama chake, na baadaye kusafirishwa kutoka jijini huko na kuletwa Dar es salaama kwa kilie kilichoelezwa na jeshi la polisi kuwa alikua na tuhuma nyingine zinazomkabili jijini humo. 

Mbowe na wenzake walisomewa mashataka sita likiwemo shataka la kutaka kufanya vitendo vya kigaidi na kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Wananchi (JWTZ). 

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti mosi na Agosti 5 mwaka 2020., hata hivyo walikana kuhusika na makosa hayo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya ambao wote ni makomandoo wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), katika kikosi cha 92 KJ kilichopo Ngerengere, waliofukuzwa kazi jeshini kutokana na sababu mbalimbali.