Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu amesema katika mazungumzo yake na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hasaan amemweleza kuwa anahitaji kurudi nyumbani lakini kabla ya kurudi anahitaji Rais Samia, atoe kauli ya kumkaribisha nyumbani(Tanzania), ili amuondoe wasiwasi kutokana na mazingira alioyoondokea tangu alivyopigwa risasi.
Jana Rais Samia alikutana na kufanya mazungumzo na Tundu Lissu Brussels nchini Ubelgiji, kufuatia maombi ya Lissu ya kutaka kuzungumza nae.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Lissu ameweka wazi mambo aliyosema kwamba ndio wamezungumza na Rais Samia, mazungumzo ambayo yameibua hisia chanya tofauti na ilivyotarajiwa.
Pamoja na Lissu kumueleza Rais Samia nia yake ya kutaka kurudi nyumbani lakini pia waliweza kuzungumzia kuhusu hali ya kisiasa nchini na kugusia kesi ya Mbowe na wenzake watatu ambapo alimwambia kuwa kesi hiyo inapaswa kufutwa kwa kuwa ni ya uongo na hainufaishi CCM wala CHADEMA, isipokuwa inazidi kuwagawa Watanzania.
Pia Lissu amewasilisha suala la mikutano ya vyama vya siasa kwamba iruhusiwe na vyama hivyo vipewe ulinzi na polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Jambo lingine ni kuhusu suala la Katiba mpya ambapo amemsihi Rais Samia kwamba hiyo ni alama na kumbukumbu kubwa anayoweza kuwaachia Watanzania.
Lissu amesema amezungumza na Rais Samia, suala la Watanzania waishio uhamishoni, kwamba Rais atamke kwamba wanakaribishwa nchini na watakuwa salama ili waweze kuridi.
Aidha Lissu ametaka wale wote waliohusika katika shambulio dhidi yake mwaka 2017 wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Pia amezungumza suala la kuvuliwa ubunge na kunyimwa stahiki zake, akieleza kwamba hayo yamefanyika kinyume na sheria.
Lakini pia amemweleza Rais kuhusu Wabunge 19 wa Viti Maalum ambao amesema kwamba hawako bungeni kihalali kwani tayari walishavuliwa uanachama wao. Lissu amesema suala la rufaa sio tiketi ya kuwaacha bungeni, na kwamba kuendelea kuwalipa fedha ni kuliibia Taifa.
Kwa mujibu wa Tundu Lissu amesema yote aliyomueleza Rais Samia kuwa ameyapokea na kwamba atayafanyia kazi.
Rais Samia yupo nchini Ubelgiji akiendelea na ziara ya kikazi aliyoianza mara baada ya kumaliza ziara yake nchini Ufaransa.