Balozi wa Kenya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Dkt George Masafu, Jumatano alikuwa katika shughuli ya kutuliza hali ya wasiwasi wa kidipolomasia uliochochewa na matamshi ya Naibu Rais William Ruto, ambayo yalionekana kudhalilisha nchi hiyo.
Mjumbe huyo Jumatano alikiri kumekuwa na “maoni hasi” baada ya matamshi ya Dkt Ruto kuhusu nchi hiyo kukosa uwezo wa kufuga ng’ombe wa maziwa.
“Ubalozi wa Kenya mjini Kinshasa, umesikitishwa na matamshi ya Naibu Rais Ruto kuhusu sekta ya kilimo ya DRC Ruto wakati wa kampeni za kisiasa nchini Kenya,” ilisomeka taarifa ya mjumbe huyo.
“Ubalozi umefahamisha Wizara ya Mashauri ya Kigeni jijini Nairobi kuhusu hisia hasi ambazo maoni hayo yamezua miongoni mwa jumuiya ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla nchini DRC,”Dkt Masafu aliongeza.
“Ubalozi wa Kenya ungependa kusisitiza kwamba serikali na watu wa Kenya wanaushirika mzuri na heshima kwa wakongo,uhusiano wa kihistoria na serikali na watu wa DRC. Uhusiano huu unaanzia kwenye uhuru wa nchi zetu,” alisema.
Katika video iliyosambazwa mitandaoni, Naibu Rais Ruto, katika mkutano wa kampeni huko Nyeri siku ya Jumatatu, anasikika akiwakejeli Wakongo kwa kuvaa suruali kiunoni na kutoweza kufuga ng’ombe kama kitega uchumi.
“Tuna soko nchini DR Congo… watu hawa ambao ni waimbaji… Watu hawa idadi yao takriban milioni 90 lakini hawana ng’ombe,” alisema, huku akitumia mfano huo kuwaahidi wapiga kura kwamba utawala wake utaimarisha uwekezaji katika ufugaji ili kuwezesha Kenya kuuza bidhaa za maziwa na nyama ya ng’ombe kwa DRC, nchi ambayo inasubiri kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia aliwataja Wakongo kama “wanavaa long’i kwa tumbo” Wanamuziki wa Kongo mara nyingi huonekana kwenye video za muziki wakiwa wamevalia suruali kiunoni.
Ingawaje maoni yake yalikuwa ya kawaida wakongo walikasirishwa.
Siku ya Jumanne, wanahabari, wanaharakati, wanasiasa na Wakongo walisikitishwa na matamshi hayo ya Naibu Rais Ruto.