BioNTech ya Ujerumani, ambayo pamoja na Pfizer ilitengeneza chanjo ya kwanza ya mRNA dhidi ya UVIKO 19, ilisema Jumatano inapanga kusafirisha vitu vya kuzalisha chanjo hiyo nchini Afrika.
“Swali lilikuwa, je tunaweza kuunda vitu hivyo viwe vidogo ili viwezekutoshea kwenye kontena,”mtendaji mkuu na mwanzilishi mwenza wa BioNTech, Ugur Sahin, aliiambia AFP wakati kampuni hiyo ilipozindua vituo vipya, vilivyopewa jina ‘BioNTiners.’
BioNTech ilisema inalenga kuanzisha “kituo cha kwanza cha uzalishaji wa chanjo katika Umoja wa Afrika” katikati ya 2022 na inatarajia kusafirisha maabara hizo ndogo za uzalishaji wa Rwanda na/au Senegal.
Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Senegal Macky Sall walihudhuria mkutano wa Usawa wa Chanjo kwa Afrika kwenye tovuti ya uzalishaji ya mRNA ya BioNTech huko Marburg, Ujerumani, pamoja na Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo na mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Tedros alisema kuwa kuongeza uzalishaji wa ndani ni muhimu haswa kwani zaidi ya nchi 100 ulimwenguni zimeshindwa kufikia kiwango cha chanjo cha asilimia 70 ambacho WHO ilikuwa ikilenga kufikia katikati ya mwaka huu.
Bara la Afrika ndilo bara lenye idadi ndogo ya watu waliochanjwa duniani — zaidi ya miaka miwili baada ya janga hili kuanza na zaidi ya mwaka mmoja baada ya kutolewa kwa chanjo ya kwanza ya virusi vya corona, chini ya asilimia 12 ya Waafrika wamechanjwa kikamilifu.
Mapema mwezi huu, kampuni ya kibayoteki ya Afrika Kusini ya Biologics ilitangaza kuwa imetoa chanjo ya kwanza ya bara la Afrika kutokana na teknolojia ya mRNA kwa kutumia kanuni za kijeni ambazo mtengenezaji mwingine wa chanjo ya mRNA, Moderna, alikuwa ametoa awali.
Sahin alisema BioNTech, ambayo ilitengeneza chanjo yake na kampuni kubwa ya dawa ya Amerika Pfizer, imeuza makumi ya mamilioni ya chanjo hiyo na ilikuwa na lengo la “kuweka vituo vya uzalishaji kwa teknolojia yetu ya mRNA katika kila bara.”