Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, ametengua uteuzi wa Kamisha Mkuu wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Salum Yussuf Ali na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Usajili, Ukaguzi na Upelelezi wa Walipa Kodi wa mamlaka hiyo, Hashim Kombo Haji, ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa shilingi bilioni 9.65.
Rais Mwinyi amechukua hatua hiyo leo wakati akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumi Uchumi Zanzibar (ZAECA), katika ofisi za ZRB, visiwani Zanzibar.
Amesema, upotevu huo wa fedha umebainika baada ya uchunguzi kufanyika katika moja ya kampuni inayosafirisha abiria kwa meli.
“Kuna uchunguzi umefanywa wa moja ya makampuni yanayosafirisha abiria kwa meli, taarifa ya malipo yaliyooneshwa ya ulipaji na taarifa za uchunguzi kunaonyesha kuna utofauti wa ulipaji wa Sh.9 bilioni. Hazikulipwa ikaonekana kwamba mhusika kalipa mfumo umechezewa fedha hazikuonekana zilikokwenda,” amesema Rais Mwinyi.
Rais Mwinyi amesema, uchunguzi umebainisha kwamba, Haji aliamuru ripoti ya fedha hizo iondolewe isipelekwe kwenye uongozi, kisha Ali akaamuru ripoti ya uchunguzi huo isipelekwe katika bodi ya ZRB.
“Taarifa hiyo imefanywa na vijana wa hapa wa uchunguzi, imeletwa hapa menejiment mnayo taarifa hiyo. Kilichotokea ni nini, kilichotokea mkurugenzi wa usjaili, ukaguzi na mpelelezi wa walipa kodi Haji aliamuri ripoti hiyo iondolewe isipelekwe kwenye menejimenti,”
Aidha ameongeza kuwa “Ripoti hiyo ikapelekwa kwenye menejimenti, kilichofuatwa ripoti haikupelekwa kwenye bodi, kwa kibali cha kamishna mkuu ikaondolewa haikupelekwa kwenye bodi. Kwa hiyo bodi mnaweza mkawa hamjui lakini kipo hicho kitu.”