Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Kamati ya uchunguzi wa mauaji ya Mtwara yaongezewa siku 7 - Mwanzo TV

Kamati ya uchunguzi wa mauaji ya Mtwara yaongezewa siku 7

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongeza siku saba kwa kamati maalum iliyopewa jukumu la kuchunguza mauaji yaliyofanyika mkoani Mtwara na Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.

Awali kamati hiyo ilipewa siku 14 kuchunguza mauaji hayo lakini kutokana na ukubwa wa kazi na mahitaji ya kujiridhisha na baadhi ya masuala, Kamati imeomba kuongezewa siku saba kuanzia Februari 17 hadi Februari 23, 2022.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa; “Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameridhia kuongeza muda wa siku saba kwa kamati maalum iliyopewa jukumu la kuchunguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi, Tanga. Kamati hiyo iliyoanza kazi Februari 4, mwaka huu, ilipaswa kukamilisha ripoti yake ndani ya siku 14, zilizoishia Februari 17.

Lakini kutokana na ukubwa wa kazi na mahitaji ya kujiridhisha na baadhi ya masuala, kamati imeomba kuongezewa siku saba kuanzia Februari 17 hadi Februari 23.”

Kamati hiyo iliundwa na Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Februari 4, mjini Magu,jijini  Mwanza akiwa njiani kuelekea Musoma, mkoani Mara kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya CCM.

Februari 4, mwaka huu Rais Samia akiwa wilayani Magu akielekea katika sherehe za maadhimisho ya miaka 45 ya CCM mkoani Mara alimwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda kamati huru kuchunguza tuhuma za mauaji mkoani Mtwara yanayodaiwa kufanywa na askari polisi.

Rais Samia alisema; “Kuna mauaji yametokea Mtwara na kwa taarifa zilizoko polisi ndio lililofanya mauaji. Taarifa niliyonayo ni kwamba polisi wameunda kamati ya kufanya uchunguzi halafu walete taarifa.”

“Haiwezekani jeshi lifanye mauaji halafu jeshi lichunguze lenyewe,” amesema Rais Samia nakuongeza.

Kutokana na hali hiyo, Rais Samia alimwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuunda kamati huru kuchunguza tuhuma za mauaji mkoani Mtwara yanayodaiwa kufanywa na askari polisi.

Baada ya agizo hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliunda kamati maalumu ya watu tisa ya kuchunguza mauaji yaliyofanywa Mtwara na Kilindi, Tanga.

Pia Waziri Mkuu alimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, awasimamishe kazi maofisa wa polisi wa Mtwara na Kilindi iii kupisha uchunguzi wakati timu aliyoiunda ikifanya kazi yake.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa mamlaka husika kuendelea kutoa ushirikiano kwa kamati ili iweze kuikamilisha kazi hiyo kwa wakati na ufanisi

Kamati hiyo ina maofisa wenye dhamana kutoka mamlaka tofauti za serikali ikiwamo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, TAKUKURU, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.