Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mtwara imewaachia kwa dhamana watu watatu walioshitakiwa mwaka 2017 kwa kosa la Ugaidi kwa madai ya kujiunga na kikundi cha Hisbu Tahir kinachodaiwa kushawishi watu kujiunga nacho na kuanzisha dola ya kiislamu nchini.
Walioachiwa ni Ramadhani Moshi Kasoko, Waziri Selemani Mkalianganda na Omar Salum Bumbo, ambao walikaa mahabusu tangu Disemba 5, 2017 baada ya kukamatwa kwa tuhuma hizo za ugaidi.
Watu hao wameachiwa baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP) kuleta ombi maalumu mahakamani hapo kutaka waachiwe kwa dhamana huku upelelezi wa kesi dhidi yao ukiendelea.
Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na kesi hizo mbele ya mahakimu wawili tofauti, walikamatwa mwaka 2017 katika maeneo tofauti tofauti ya mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara, kisha kushitakiwa katika kesi namba 09/2017. Hadi wanaachiwa, upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa haujakamilika.
Hakimu Mkazi, Musa Esanju alisema kuwa washitakiwa hao wameachiwa kwa baada ya kutimiza vigezo vya dhamana ambayo ni pamoja na kila mmoja wao kuwa na wadhamini wawili wenye kiasi cha Sh20 milioni kila mdhamini.
Hakimu Esanju amewaambia waandishi wa habari kuwa baada ya Jamhuri kujiridhisha kuwa wametimiza vigezo vya kupewa dhamana washtakiwa hao wameachiwa.
Miongoni mwa masharti ya dhamana yao ni kutoa ahadi ya kutunza amani na kuonesha tabia njema kwa muda wa miaka mitatu wakiwa chini ya uangalizi.
Vile vile wametakiwa kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) mkoa wa Mtwara Kila ijumaa ya mwisho wa mwezi kwa miaka mitatu.
Washtakiwa hao watakuwa chini ya uchunguzi na uangalizi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakifatiliwa nyendo zao na iwapo watavunja makubaliano hayo, kesi dhidi yao itahuishwa.