Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema kuwa hadi sasa hakuna Mtanzania aliyepata madhara yoyote kufuatia hali inayoendelea nchini Ukraine na kusababisha Serikali ya nchi hiyo kutangaza hali ya hatari Februari 24.
Aidha Serikali ya Tanzania imewaomba wananchi wote wanaoishi nchini Ukraine ikiwemo wanafunzi, Wafanyabiashra na Wafanyakazi kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hichi ambacho Serikali hiyo inaendelea kufuatilia usalama wao kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za nchini Ukraine.
Kadhalika kufuatia kutangazwa kwa hali hiyo ya hatari Serikali imewashauri Watanzania wanaoishi Ukraine kufata na kutekeleza maelezo yote yanayotolewa na Serikali ya Ukraine kwa raia wasiokuwa raia wa nchi hiyo.
Pia imewasisitiza raia wake kuendelea kuwasiliana na ubalozi wa Tanzania nchini Sweden ambao pia unawakilisha Ukraine kwa jambo lolote la dharura kwa kufuata utaratibu wa mawasiliano uliotolewa na ubalozi huo.
Aidha kwa upande wa Wanafunzi waliopo Ukraine wametakiwa kufuata maelekezo na miongozo wanayopewa na uongozi wa vyuo vyao, ikiwa ni pamoja na wazazi wa wanafunzi hao kuwasiliana na watoto wao ili kukubaliana utaratibu wa kuwarejesha pale itakapobidi kufanya hivyo.
Kwa sasa Serikali ya Tanzania ianendelea kufuatailia kwa ukaribu kuhusu hali za Watanzania waliopo Ukraine na inatoa rai kwa wazazi wa wanafunzi wanaosoma Ukraine kuwa watulivu sambamba na kuwataka Watanzania wote wanaoishi nchini humo kufuta miongozo na maelekezo inayotolewa na Ukraine.
Mashambulizi ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine yamewashangaza wengi huku wengine wakitamani kujua nguvu za kijeshi za mataifa hayo ya Ulaya Mashariki ambayo yamekuwa kwenye mgogoro kwa miaka kadhaa.
Takwimu zilizotolewa usiku wa jana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky zinaonyesha kwamba watu 137 wameuawa kwenye mashambulizi hayo na wengine 316 wakijeruhiwa.