Mfalme Zumaridi ni nani?

Jeshi la Polisi  jijini Mwanza linamshikilia Diana Bulamba maarufu ‘Mfalme wa Zumaridi’(39) mkazi wa Mtaa wa Buguku, Kata ya Buhongwa kwa tuhuma ya usafirishaji haramu wa binadamu  149  na unyonyaji.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ramadhan  Ng’anzi, jana Jumapili alisema kuwa, tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 6:30 mchana katika Mtaa wa Buguku, Kata ya Buhongwa Wilaya ya Nyamagana.

Alisema watu hao waliosafirishwa 57 ni wanaume na 92 ni wanawake, wakiwemo watoto 24 wenye umri wa miaka kati ya minne hadi 17 na wametolewa kutoka sehemu mbalimbali na kisha kuwafungia nyumbani kwake na kuwatumikisha.

“Watoto hao ni wale waliokatizwa masomo yao kinyume cha sheria na amekuwa akiwahadaa kuwa yeye ni Mungu anayeponya, kufufua watu na kutatua matatizo yao,” alisema 

Aidha Kamanda Ng’anzi alisema mtuhumiwa huyo alibainika baada ya Februari 23, mwaka huu polisi kupokea amri ya Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni iliyowataka kumkamata mzazi wa kike wa mtoto Samir Abbas aliyetakiwa kufikishwa mbele ya mahakama hiyo baada ya kesi ya msingi kusikilizwa katika mahakama hiyo.

“Katika utekelezaji wa amri hiyo, polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa Dianna Bundala ambapo ilidaiwa yupo mzazi wa kike wa mtoto huyo na mtoto aliyetakiwa kufikishwa mahakamani, lakini kwa mshangao mtuhumiwa akiwaongoza wafuasi wake waliwashambulia askari na kuwazuia kufanya kazi yao,” alisema.

Baada ya tafrani hiyo askari polisi waliondoka eneo la tukio kwa nia ya kuepusha kutotumia nguvu ambayo ingeweza kusababisha madhara na baadaye Februari 26, mwaka huu walirudi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na kufanikisha ukamataji kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo upelelezi wa kina wa tukio hilo bado unaendelea ili kubaini kiini cha watu hao kukusanyika katika nyumba ya mtuhumiwa ambayo siyo ya ibada wala sehemu rasmi ya kongamano.

Je Mfalme Zumaridi ni nani?

Mwaka 2019 alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na alivyokuwa akiendesha ibada huko jijini Mwanza tofauti na makanisa mengine yanavyoendesha ibada.

Aina yake ya uendeshaji wa ibada ulikuwa gumzo kwani Mfalme Zumaridi haamini katika aina yeyote ya dini hali inayoleta maswali hadi sasa.

Ana wafuasi wengi wanaomuamini, na wanamwamini `Mfalme Zumaridi’ kama mwakilishi wa Mungu duniani ama `Yesu Kristo’ wa duniani.

Wakati huo wafuasi wake  hulala chini huku mchungaji wao akiwakanyaga na kupita juu yao, wakati mwingine waumini wa kanisa hilo pia huonekana wakigaragara kwenye matope ya majaruba ya mpunga jirani na kanisa lao kama moja ya ibada ikiwa ni ishara ya kumshughulikia shetani.

Hata hivyo baada ya kuonekana video mbalimbali za mahubiri yake kanisani kwake, Serikali iliingilia kati na ndipo ikachukua uwamuzi wa kulifungia kanisa la Mfalme Zumaridi, ambapo pia iliamuru kutofanyika ibada kanisani hapo wala nyumbani kwa Mfalme Zumaridi.

Hatua hii pia ilikua ni baada ya uchunguzi kubaini kuwa baadhi ya maneno na matendo yyalikuwa yakifanyika kanisani kwa Mfalme Zumaridi yalikuwa na athari na madhara kwa waumini na watu wengine pamoja na umnwepo wa malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wa taasisi zingine za kidini kuhusu ukiukwaji wa sheria, maadili na imani ya kidini.