Nigeria, Afrika Kusini na serikali nyingine za Afrika ziling’ang’ana Jumatatu kusaidia raia wao kuepuka uvamizi wa Urusi nchini Ukraine baada ya ripoti za ubaguzi wa rangi na kutotendewa haki kwa Waafrika kwenye vivuko vya mpaka.
Waafrika nchini Ukraine, wengi wao wakiwa wanafunzi, ni miongoni mwa mamia ya maelfu ya watu wanaojaribu kukimbilia Poland na mataifa mengine jirani.
Viongozi wa Umoja wa Afrika walielezea wasiwasi wao kutokana na ripoti za unyanyasaji wa Waafrika waliopatikana katika mzozo wa Ukraine na kusema tabia kama hiyo itakuwa ‘ya ubaguzi wa rangi’.
Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, Rais wa Senegal Macky Sall, na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat walisema Jumatatu kwamba ‘wamesikitishwa hasa na ripoti kwamba raia wa Afrika katika upande wa mpaka wa Ukraine wananyimwa haki ya kuvuka mpaka’.
“Ripoti kwamba Waafrika wanatengwa kwa kutendewa tofauti ni ubaguzi wa rangi na kukiuka sheria za kimataifa,’ walisema katika taarifa.
“Nchi zote zinapaswa “kuheshimu sheria za kimataifa na kuonyesha huruma sawa na kutoa msaada kwa watu wote wanaokimbia vita bila kujali asili yao au rangi” aliongeza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Godfrey Onyeama alisema Jumatatu kuwa uhamisho wa raia wa nchi hiyo utaanza Jumatano.
Hapo awali, mshauri wa rais Garba Shehu alikuwa amewataka maafisa wa mpaka wa Ukraine kuwatendea raia wa Nigeria kwa usawa baada ya ripoti kuwa wamezuiwa kupanda mabasi na treni hadi mpakani.
Shehu alizungumzia video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha mama mmoja wa Nigeria akiwa na mtoto mchanga akilazimishwa kuondoka kutoka kwa kiti alichoketia.
Kumekuwa pia na ripoti za maafisa wa Poland kukataa raia wa Nigeria kuingia Poland kutoka Ukraine, aliongeza.
“Wote wanaokimbia hali ya migogoro wana haki sawa ya kupitishwa kwa usalama chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na rangi ya pasipoti zao au ngozi zao hazipaswi kuleta tofauti,” alisema Shehu.
Wakae nje
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini Clayson Monyela wakati huo huo alitweet kwamba kundi la raia wa nchi yake, hasa wanafunzi, wamekwama kwenye mpaka wa Ukraine na Poland.
Balozi wa Afrika Kusini huko Warsaw alikuwa kwenye mpaka akijaribu kuwapata, aliongeza.
Siku ya Jumapili, Monyela alisema Waafrika ‘wanatendewa vibaya’ katika mpaka wa Poland na Ukraine.
Balozi wa Poland nchini Nigeria Joanna Tarnawska alipuuzilia mbali madai ya kutotendewa haki.
“Kila mtu anatendewa sawa. Ninaweza kukuhakikishia kwamba nina ripoti kwamba tayari baadhi ya raia wa Nigeria wamevuka mpaka na kuingia Poland,” aliambia vyombo vya habari vya ndani.
Raia wa Nigeria wanaweza kukaa kwa siku 15, na hata hati batili zilikuwa zinakubaliwa kuvuka mpaka na vizuizi vya Covid-19 viliondolewa, alisema.
Baadhi ya Wanigeria waliovuka mipaka walieleza kuwa walisubiri huku maafisa wakitoa kipaumbele kwa wanawake na watoto wa Ukraine.
“Mmoja wa maafisa alikuja na kutuambia ni vigumu zaidi kwa sisi wageni kwa sababu wanapaswa kuwasiliana na serikali yetu katika nchi tofauti,”Stephanie Agekameh, mwanafunzi wa matibabu nchini Poland, alisema kwa ujumbe wa simu.
Akizungumza kutoka Korczowa nchini Poland, mwanafunzi wa sayansi ya usimamizi wa Nigeria Agantem Moshe, alisema polisi wa Ukraine wamewasukuma Waafrika kutoka njiani kutoa nafasi kwa wanawake na watoto wa Ukraine,
“Kutoka upande wa Poland ilikuwa shwari, walikuwa wataalamu. Huko Ukraine, walituweka nje kwenye baridi,”alisema.
Umoja wa Mataifa ulisema kuwa zaidi ya wakimbizi nusu milioni kutoka Ukraine hadi sasa wamevuka hadi nchi jirani.
Ubalozi wa Nigeria mjini Bucharest ulisema umepokea Wanigeria 130 kutoka Ukraine, huku wengine wakishughulikiwa wakiwa wamefika Warsaw au Budapest.
‘Kipaumbele kwa Waukraine’–
Serikali ya Ghana ilisema kuwa itakutana na wazazi wa wanafunzi waliokwama nchini Ukraine siku ya Jumanne na kutuma maafisa wa ubalozi kwenye maeneo ya mpakani kusaidia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Christophe Lutundula alisema kwenye Twitter kwamba atakutana na balozi wa Poland kusaidia kuvuka mpaka wa takriban Wakongo 200, wengi wao wakiwa wanafunzi.
Ivory Coast, ambayo kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ina raia 500 nchini Ukraine, ilisema pia inafanya mipango ya kuwahamisha.
Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Kenya ilisema juma lililopita takriban Wakenya 200 walikuwa salama na wamepatikana lakini baadhi yao walikwama katika mpaka wa Poland kwa sababu ya vikwazo vya viza.
Mhasibu wa Nigeria Lukmon Busari alisema mwanawe, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa udaktari, alikuwa ashavuka mpaka baada ya kusubiri kwa siku moja kwenye mpaka wa Poland.
“Mwanzoni hawakuwaruhusu kuhama kwani waliwapa kipaumbele Waukraine, hususan wanawake na watoto. Hatimaye waliwaruhusu kuingia Poland,” Busari aliiambia AFP kwa njia ya simu.
Kulingana na yeye, mamlaka ya Kipolishi “ilifanya kazi nzuri.”