Umoja wa mataifa na wadau wa masuala ya kibinadamu wamezindua ombi la dharura la jumla ya dola bilioni 1.7 ili kufikisha haraka msaada wa kibinadamu kwa watu nchini Ukraine na wakimbizi waliokimbilia nchi jirani
Ombi hilo lililozinduliwa jana mjini Geneva, nchini Uswis na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA na lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR limefuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine yaliyosababisha mahitaji makubwa ya kibinadamu baada ya huduma muhimu kuathirika na maelfu ya watu kufungasha virago kuzikimbia nyumba zao kwenda kusaka usalama.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu milioni 12 ndani ya Ukraine watahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi huku wengine zaidi ya milioni 4 wakimbizi wa Ukraine watahitaji ulinzi na msaada katika nchi jirani waliko kimbilia katika miezi ijayo.
Mkuu wa OCHA Martin Griffiths amesema Familia zilizo na watoto wadogo zimejificha kwenye mahandaki na treni za chini ya ardhi au zimelazimika kukimbia milio ya kutisha ya mmilipuko na sauti yza magari ya wagonjwa au ya zimamoto.
Idadi ya majreruhi na vifo inaongezeka kwa kasi, wakati ambao unatajwa kuwa ni mbaya zaidi kwa watu wa Ukraine.
“Tunataka kuongeza operesheni zetu sasa ili kulinda Maisha na utu wa watu wa Ukraine. Tunapaswa kuchukua hatua kwa utu na mshikamano.”amesema Mkuu wa OCHA Martin Griffiths
Dola bilioni 1.1 za ombi hilo zitatumika kuwasaidia watu milioni 6 ndani ya Ukraine kwa miezi mitatu na msaada unajumuisha ugawaji wa fedha taslim, chakula, maji na usafi, huduma za afya, elimu , malazi na kukarabati nyumba zilizobomoka na makombora.
Pia fedha zingine zitasaidia mamlaka ili kuhakikisha vituo vilivyopo na vipya vitakavyoanzishwa kwa ajili ya watu waliotawanywa.
Naye mmkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema “ Tunaangalia ambacho kinaweza kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi barani Ulaya katika karne hii. Wakati tunashuhudia mshikamano na ukarimu wa hali ya juu kutoka nchi Jirani katika kuwapokea wakimbizi, msaada Zaidi unahitajika kuwasaidia na kuwalinda watu wapya wanaokimbia.”
Mkakati wa kikanda wa kusaidia wakimbizi RRP unahitaji dola milioni 550.6 ili kusaidia wakimbizi wa Ukraine Poland, Moldova, Hungary, Romania na Slovakia, lakini pia katika nchi nyingine kwa malazi, fedha, na msaada wa kisaikolojia kwa waliokimbia wakiwemo wenye mahitaji maalum kama watoto wanaokimbia bila wazazi au walezi.