Viongozi wa dini nchini Tanzania wamemuomba Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan kutumia busara ili kuweza kuimaliza kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu
Hayo yamejiri jana Ikulu jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa viongozi wa dini na Rais Samia Suluhu ikiwa ni mwendelezo wa ahadi ya rais huyo katika kukutana na makundi mbalimbali kuzungumza nayo.
Viongozi hao wamesema kuwa hawataki kuingilia muhimili wa sheria lakini kwa kutumia mamlaka aliyonayo rais wameomba Mbowe na watuhumiwa wengine wa kesi za ugaidi waachiwe kutokana na wengine kukaa muda mrefu magerezani pasipo ushahidi kukamilika.
Shekhe Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakar Bin Zuberi, alimwambia Rais Samia kuwa Suala la Mbowe linahitaji huruma na busara kutumika ili kulimaliza.
“Huruma zako zinahitajika zaidi na sisi tunaona mama ni mwepesi wa huruma kuliko baba.Hili jambo ni zito linahitaji hekma na busara ijitokeze kuwahurumia hawa watu wawe huru bila ya sisi kuingilia mambo ya Mahakama, halafu tuangalie katika kukosa kwao mara ya kwanza watatulia? wataelewa somo?
Mufti Abubakari ameongeza kuwa “Sisi kama viongozi wa dini tunaona hili jambo tulifikishe kwako, tukushauri tukuombe pia uwafanyie huruma, huruma jambo la mana sana”
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Jackson Sostenes amesema hata Mungu husamehe na pia sheria siyo mwisho wa kufikiri hivyo amemuomba Rais Samia kulishghulikia suala hilo.
“Katika kesi ya ndugu yetu Mbowe, katika muktadha wa hilo ambalo linaendelea sitaki kuingilia muhimili wa sheria lakini kuna busara inasema sheria siyo mwisho wa kufikiri” amesema Askofu Jackson
Ameongeza kuwa “Kwa hiyo kwa tafsiri hiyo ningeshauri busara ya serikali yetu ione namna ya kulishghulikia ambayoi italeta afya zaidi kwa mapenzi mapana ya taifa hata kama sheria inazungumza kitu gani.”
“Sisi viongozi wa dini tunasema msifanye hivi msifanye hivi, pamoja na sheria bado kuna sala ya toba na Mungu pia hutoa msamaha, kwa hiyo tulidhani kuwa ikionekena inafaa na haina athari kubwa kwenye taifa basi kama kiongozi mkuu mlimalize kwa busara na hekma”
Itakumbukwa kuwa haya yanajiri ikiwa imebaki siku moja Mbowe na wenzake kuanza kujitetea mahakamani katika kesi ya Ugaidi inayowakabili.
Si viongozi wa dini pekee wanaitaka ama kuiomba Serikali imwachie Mbowe bali Wanaharakati, Viongozi wa vyama vya siasa za upinzani, na hata wanachama wa CHADEMA mara kadhaa wamekuwa wakiitaka Serikali iliyopo mamlakani imwachie Mbowe na wenzake huku wengi wakisema Mbowe sio gaidi.
Februari 18 siku ya Ijumaa Mbowe na wenzake watatu walikutwa na kesi ya kujibu katika kesi ya Ugaidi inayowakabili.
Mbali na Mbowe wengine ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya