Serikali ya Tanzania leo imepokea dawa za kukinga minyoo kwa watoto Albendazole milioni nane zenye thamani ya shilingi milioni 550
Dawa hizo zimetolewa na Shirika la Wolrd Vission Tanzania na Canada, zitaanza kugawiwa kwa watoto hao kwenye kampeni maalumu inayotarajiwa kufanyika Juni na Julai mwaka huu.
Msaada huo umepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Naibu Waziri wa Afya nchini humo, Dk Godwin Mollel wakati wa hafla ya kupokea dawa hizo iliyofanyika katika maghala ya Bohari ya Dawa (MSD).
Naibu Waziri Afya amesema kampeni hiyo ambayo imekuwa ikifanyika mara mbili kwa mwaka Desemba na Juni, husaidia watoto wasiwe na upungufu wa damu, minyoo na kuwa na viini lishe vinavyokwenda kujenga ubongo wa mtoto.
“Tumepokea kitu muhimu sana na dunia ya leo haishindani kwa rasilimali kubwa bali kwa watu wenye akili hivyo hii dawa tunakwenda kutengeneza usalama wa akili za watoto wetu” Amesema Dk Mollel
“Kimsingi hili tusichukulie tu kama dawa bali tuchukulie zaidi ya dawa na tunapozungumzia masuala ya lishe siyo kushiba sababu wazazi wengi wanachanganya kati ya shibe na lishe ukiwaambie mkalishe watoto wanaenda kuwajaza uji na ugali tumboni”- Ameongeza
Mjumbe wa Board ya World Vision, Diana Rugaitika alisema kipaumbele cha shirika hilo ni usalama wa mtoto, afya zao na elimu yao alisema walipata nafasi kuchangia dawa hizo mwanzoni mwa mwaka kwa dawa za shilingi milioni 340 zikiwamo vitamin A na hii ni awamu ya pili.
“Baada ya kuona bado kuna upungufu leo tumepata nafasi tena ya kurudi kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa msaada huu ili kuhakikisha watoto wetu wanakuwa na afya njema”
“World Vision Tanzania tukishirikiana na Canada tumeleta Albendazone milioni 8 zinazogharimu shilingi milioni 550 ambayo tunaamini itaziba kwenye ule upungufu uliokuwepo lakini tunaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya ili kuhakikisha watoto wetu wanakuwa na afya,” amesema Rugaitika.
Kwa upande wake Balozi Mulamula amesema, “World Vision mmekuwa ni wadau wetu mpo maeneo mtambuka na mmekuwa mkitusaidia katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama kiafya, lakini mpo kwenye maeneo mengine na mmetujengea jina nilipokuwa balozi Marekani walikuwa wakisema World Vision Tanzania mko vizuri sana.”