Hukumu rufaa ya Sabaya na wenzake kutolewa Mei 6

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha inatarajia kutoa hukumu ya rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili wanaopinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Hii leo rufaa hiyo ya jinai namba 129/2021 ilipangwa kwa ajili ya kutajwa ambapo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Ruth Massam amesema hukumu hiyo itatolewa Mei 6, 2022.

“Tumefikia mwisho wa usikilizwaji wa shauri na kama ambavyo awali niliwaeleza hili shauri lilipangwa kusikilizwa kwa mfumo wa session na muda ambao ulipangwa umemalizika. Shauri litakuja kwa ajili ya mention (kutajwa) Machi 15 na itapangwa uamuzi unatolewa lini,” alisema Jaji Kisanya Februari 21, 2022 wakati wa kuhitimisha usikilizaji wa rufaa hiyo.

Rufaa hiyo iliyoanza kusikilizwa mfululizo Februari 15 mwaka huu inatokana na shauri la awali la jinai lililokuwa namba 105, 2021 lililokuwa likiwakabili Sabaya na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Katika rufaa hiyo waomba rufaa hao walikuwa wakilishwa na Mawakili Mosses Mahuna, Fauzia Mustafa, Sylvster Kahunduka, Edmund Ngemela na Fridolin Bwemelo ambao kwa pamoja walipinga hoja za wajibu rufaa na kuomba mahakama iridhie hoja zao 14 za rufaa na kuwaachia wateja wao huru.

Upande wa Jamhuri uliwasilishwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Ofmedy Mtenga, Verediana Mlenza na Wakili wa Serikali Baraka Mgaya, ambao walipinga hoja hizo za mawakili wa waomba rufaa na kuomba mahakama itupilie mbali rufaa hiyo.

Oktoba 15 ,2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo aliwahukumu Sabaya na wenzake wawili kifungo cha miaka 30 kila mmoja, baada ya kukutwa na hatia katika makosa matatu ikiwamo unyang’anyi wa kutumia silaha.

Hukumu hiyo iliyosomwa zaidi ya saa sita kuanzia saa 5:57 asubuhi ambapo,katika hukumu hiyo Hakimu Amworo, alisema kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa mahakamani, aliridhika washitakiwa hao walimpora Numan Jasin, Bakari Msangi na Ramadhan Rashid.

Katika kosa la kwanza ilidaiwa Februari 9, 2021 Mtaa wa Bondeni, Arusha, washitakiwa hao waliiba shilingi milioni 2.769 mali ya mfanyabiashara Mohamed Saad.

Katika shitaka la pili, Sabaya na wenzake walidaiwa kuiba shilingi 390,000 mali ya Msangi, wakiwa katika duka hilo la Mohamed ambapo pia walidaiwa kumfunga pingu, kumpiga na kumshambulia huku wakimtishia kwa bunduki kabla ya kufanya tukio hilo.

Katika shtaka la tatu, Sabaya na wenzake walidaiwa kuiba shilingi 35,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno kutoka kwa Ramadhan Rashid wakiwa katika mtaa huo.

Mbali na Sabaya waomba rufaa wengine ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura ambapo rufaa hiyo ilikuwa inasikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Sedekia Kisanya.