Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limewakamata watu wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya ‘ujambazi’ ‘unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es saalam, Jumanne Murilo amesema watuhumiwa hao wamewakamata kufuatia kufanya muendelezo wa operesheni kali iliyoanza tangu tarehe 16/3 hadi 20/03 mwaka huu ambayo imeoongozwa na taarifa fiche.
Kamanda Muliro amesema watu hao hutumia Pikipiki kutekeleza matukio hayo ya kihalifu katika jiji la Dar es Salaam.Watuhumiwa hao ni Mussa Abdulrashid (28), Mmakonde,Mkazi wa Vikindu na Tuangoma Temeke na Erick Joseph Mfuko (32), Muha,Mkazi wa Kibamba.
Aidha Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na bunduki aina ya Pistol mbili Browning namba za usajili TZCAR 113805 na Glock 15 nambari TZCAR 9611 zikiwa na risasi sita kwenye Magazine pia Pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 123 DAL ambayo wamekuwa wakiitumia kufanya uhalifu imekamatwa.
“Watuhumiwa hawa wamekiri kuhusika na matukio mbalimbali tangu Mwaka 2021 kwa kuwafuatilia kwa nyuma na Pikipiki yao baadhi ya watu waliochukua pesa zao kutoka benki ya CRDB Kibada, CRDB Pugu Road, NMB Banana, CRDB Temeke, NMB Airport na Kampuni ya ASAS zote za Dar es Salaam”– amesema Kamanda Muliro
Pia amesema mmoja wa watuhumiwa hao miaka ya nyuma Mwaka 2018 amewahi kukamatwa kupelekwa Mahakamani na gerezani kwa tuhuma za unyang’anyi.
Kamanda Muliro amesema baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa wamekiri kuhusika na matukio hayo na mahojiano kwa kina bado yanaendelea ambapo pia ametoa onyo kwa mtu au vikundi vya watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja.
Amesema Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwakamata pia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.