Wakati sakata la kumtaka msanii Steven Mengele maarufu Steve Nyerere, kujiuzulu nafasi ya usemaji wa Shirikisho la Muziki Tanzania (SMT), likipamba moto mwenyewe amesema hatojiuzulu hadi aandikiwe barua na waliomteua.
Steve ameyasema hayo leo ambapo ameweka msisitizo kuwa hatajiuzulu hadi pale waliomteua watakapompa barua kama walivyofanya wakati akitaka atumikie nafasi hiyo.
“Mimi siwezi kung’oka kihuni huni, kwa kuwa nafasi hii nimeteuliwa tena kwa barua, halafu anakuja mtu anasema anatoa saa 48 nijiuzulu. Yeye nani sitafanya hivyo labda uongozi unipe barua ya kutengua nafasi yangu,” amesema Steve.
Katika hatua nyingine msanii huyo ambaye alikuwa akisema anazungumza kama msemaji wa Shirikisho hilo amewapa saa 48, wasanii waliotoa maoni yao jana kwa dhihaka ikiwemo kuuita uongozi ‘Zumaridi Gang’ kuomba msamaha.
Katika suala hilo, wapo wanaokubaliana na uamuzi wa bodi wa Steve kuwa msemaji wao huku wengine wakimkataa na kutoa saa 48 kwa uongozi wa shirikisho hilo kumuondoa katika nafasi hiyo.
Wakitoa maoni yao hapo jana, baadhi ya wasanii walioneka kuwa na hasira na kuwa patachimbika msanii huyo asipoondolewa na wengine wakisema wamedharauliwa kwa kiwango kikubwa kuwekewa mtu asiyejua namna walivyoupigania muziki wao na wala hajui changamoto wanazopitia.
Mmoja wa waliopinga uteuzi huo ni mbunge wa Muheza, Hamisi Mwinjuma “MwanaFA” ambaye pia ni msanii wa muziki wa Hip hop. Amesema kwa katiba ya shirikisho, Steve hana sifa ya kupewa nafasi hiyo ikiwemo kutokuwa mwanamuziki.
Sakata la kutaka Steve Nyerere aondolewe katika nafasi hiyo lilianza wiki iliyopita mara tu baada ya kutangazwa na uongozi wa Shirikisho hilo na jana katika kikao cha kupokea maoni kwa wanachama kuhusu maamuzi hayo.