Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa, kuhakikisha alama ya madini ya Tanzanite inawekwa kwenye daraja la Tanzanite ili kuendana na uhalisia wa jina lake badala ya alama ya mwenge uliowekwa hivi sasa
Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akifanya uzinduzi wa daraja la Tanzanite lililopo eneo la Salender jijini Dar es salaam.
“Ushauri niliopata kwa wananchi daraja hili tunaliita la daraja la Tanzanite lakini alama tuliyoiweka ni alama ya Mwenge (wa Uhuru). Pamoja na kutambua mwenge ni tunu yetu adhimu, wananchi wangependa sana kuona umbo la Tanzanite pale ulipo Mwenge ili kukamilisha jina la daraja hili,” amesema Rais Samia.
Daraja hilo lilianza kutumiwa Februari 1 mwaka huu ambapo liliwekewa alama ya Mwenge wa Uhuru katika moja ya nguzo zake ili kutambua tunu hiyo muhimu katika maendeleo ya Tanzania.
Rais Samia amesema daraja hilo ni muendelezo wa uboreshaji wa miundombinu ya usafiri jijini humo ili kuchagiza shughuli za uzalishaji na biashara kufanyika bila vikwazo.
“Tukipunguza muda wa watu kukaa barabarani maana yake tunaongeza muda wa watu kufanya kazi. Lakini pia kupunguza gharam za mafuta yanayotumiwa na vyombo vya usafiri. Nadhani tutapunguza migogoro majumbani kwa watu kuchelewa kwa kusingizia foleni,” amesema Rais Samia.
Daraja la Tanzanite limekatiza katika Bahari ya Hindi kwa kuunganisha barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Barack Obama lina urefu wa kilomita 1.30 na barabara unganishi kilomita 5.2 ambapo limegharimu fedha za Kitanzania shilingi bilioni 243 hadi kukamilika kwake.
Ujenzi wa daraja hilo ulianza mwaka 2018, ambapo kazi ya usanifu ilikuwa imekamilika na kazi zilianza kwa kuchimba msingi ambapo nguzo zaidi ya 200 zimeingia chini ya bahari.
Ni mojawapo ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Tanzania katika kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka katika jiji la Dar es Salaam.
Pamoja na kuonekana kuwa kivutio cha utalii, pia limetajwa kupunguza msongamano wa magari jijini humo kwa sababu kwa sasa linapitisha magari kati ya 17,726 hadi 19,764 kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa.