Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wengine wakuu wa nchi na serikali kutoka kambi ya nchi za Magharibi wanakutana hii leo kujadili namna ya kuongeza shinikizo dhidi ya Rais Vladmir Putin wa Urusi.
Aidha viongozi hao pia watajadili kuhusu hali ya kuporomoka kwa uchumi na usalama inayoshuhudiwa kote barani Ulaya na duniani kwa ujumla.
Rais huyo wa Marekani atahudhuria mkutano wa jumuiya ya kujihami ya NATO, mkutano wa kundi la nchi 7 zenye uchumi mkubwa kiviwanda G7 na mkutano wa kilele wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya, mikutano ambayo yote inayofanyika leo mjini Brussels.
Biden aliyewasili jana usiku Brussels anatarajia kuwatia msukumo washirika wake kuweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi ambayo tayari uchumi wake umeanza kuathirika kutokana na vikwazo mbalimbali pamoja na hatua ya kususiwa katika kipindi cha wiki nne zilizopita.