Watu 26,800 wamefariki kwa ugonjwa wa kifua kikuu nchini Tanzania katika kipindi cha mwaka 2021, ambapo ni sawa na vifo 78 kila siku.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu na kwamba idadi hiyo imeshuka kutoka vifo 88 kwa siku kama ilivyokua mwaka 2020, huku akiongeza kuwa zaidi ya asilimia 36 ya vifo vya watu wanaoishi na UKIMWI vinasababishwa na Kifua Kikuu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi makubwa ya ugonjwa wa TB ambazo zinachangia 87% ya wagonjwa wote duniani. Kwa mujibu wa WHO ya mwaka 2021 kulikua na wagonjwa mil. 9.9 na wagonjwa mil. 1.4 sawa na 14% waliofariki
Waziri Ummy ametaka vikwazo visiwekwe kwa wagonjwa wa kifua Kikuu wanapoenda katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata matibabu.
“Dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kumfikia kila mwananchi kupata huduma za Kifua Kikuu, Serikali itahakikisha watu wenye kifua Kikuu wanapatiwa matibabu bure. Tuje na mpango wa kuwasaidia wenye Kifua Kikuu Sugu” – Amesema Ummy