CUF wapinga suala la Katiba Mpya kushughulikiwa baada ya uchaguzi wa 2025

Baraza la Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, limepinga pendekezo la kikosi kazi kuhusu suala la katiba mpya kushughulikiwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa madai kwamba, hakuna mjumbe aliyependekeza hivyo

Akizungumza kwa niaba ya baraza hilo Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliofanyika hivi karibuni jijini Dodoma, uliibuka na mapendekezo zaidi ya 80 likiwamo la uhitaji wa haraka wa katiba mpya.

“Kikosi kazi kilichoundwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji, kilikuwa na kazi ya kuchambua maoni yetu na kisha kuyarejesha kwetu wadau wenyewe, lakini ajabu ni kwamba na chenyewe kinajipa jukumu la kutoa mapendekezo,” alisema Prof. Lipumba.

Baraza hilo linasikitishwa na hatua zilizochukuliwa na kikosi kazi hicho, na kwamba ni vyema serikali na wadau wote wajue CUF na wajumbe wote wa mkutano huo walitamani katiba mpya ipatikane haraka.

Prof. Lipumba alisema, kikosi hicho kilitakiwa kuchambua mapendekezo kwa kuangalia yanayofanana na kuyaweka kundi moja na siyo kutoa mapendekezo mengine zaidi ya yale yaliyopendekezwa na wajumbe wa mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Machi 21 Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Prof. Rwekaza Mukandala aliwasilisha mapendekezo kwa Rais Samia Suluhu ambapo alitaja sababu kadhaa za kupendekeza mchakato wa katiba mpya kuanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Prof. Mukandala alitaja baadhi ya sababu kuwa ni uwapo wa haja ya kuainisha dira mpya ya maendeleo ya 2063 itakayotoa mwelekeo wa katiba mpya na suala la kukosekana kwa muda wa kutosha kuanza kutumia katiba mpya ndani ya kalenda ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Nyingine ni kutoa fursa kwa marekebisho ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa na haja ya kutoa fursa ya kutosha kufanyia kazi masuala ya muda wa kati ikiwamo kuainisha dira mpya ya maendeleo.

Aidha, alisema kuna changamoto mbili, anazoziona, ikiwamo ya watu wanaosema hakuna haja ya kuwa na katiba mpya na kwamba inaweza kufanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya sasa na baadaye, lakini ya pili kuna wale wanaodai kwamba, mchakato wa kupata katiba inayopendekezwa unze haraka.