Othmani:Sheria ya Uchochezi inatoa fursa kutumika vibaya

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema sheria ya uchochezi inatoa fursa kutumika vibaya na vyombo vinavyosimamia sheria hasa Polisi na kwamba wakati umefika wa kuifanyia mapitia ili kulinda uhuru wa kujieleza na wa habari nchini

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, aliyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wanasheria kuhusu uhuru wa habari, uhuru wa kujieleza na mashauri ya mahakama yanayohusu uhuru huo.

Othman ambaye ni mwanasheria aliyebobea, amewahi kuwa mwendesha mashtaka mkuu Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, amesema sheria hiyo kama ilivyo hivi sasa “ina mianya mingi ya kutumika vibaya” na “inaweza kukwaza sio tu uhuru wa habari bali pia uhuru kwa ujumla wake”.

Aliwaambia wanasheria na wanahabari kuwa tume za sheria za nchi nyingi zimefanya mapitio makubwa kuhusu mipaka, viini na vitendo mahsusi vinavyosababisha kosa la uchochezi na utafiti uliofanyika unaweza kusaidia Tanzania kudurusu sheria zake.

Othman alisema uzoefu wake kama mwendesha mashtaka umemwaminisha kuwa sheria za uchochezi ni kikwazo kwa uhuru wa habari.

“Najua kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya habari kwa waandishi ni wanasiasa na viongozi wa kisiasa. Mwandishi anaweza kuingia matatani pale atakaporipoti matamshi halali ya mwanasiasa na vyombo vya sheria vikatafsiri matamshi hayo kama uchochezi,” alifafanua.

Alilitaka Baraza la Habari Tanzania (MCT) kama mtetezi wa uhuru wa habari kuanzisha mjadala mpana kuhusu vifungu vya sheria vinavyohusu uchochezi.

“Lililo muhimu ni kwa kila upande kutekeleza wajibu wake na inapobidi kukosoa, kufanyike kwa misingi ya ukweli na haki kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya, tukizingatia kwamba sote tunajenga nyumba moja imara, itakayoheshimu haki na uhuru wa habari na kujieleza,” alisisitiza Makamu wa Kwanza wa Rais.

.

Othman alisisitiza kuwa ni muhimu sheria za Tanzania zizingatie Ibara za 18 za katiba zote, ile ya Muungano na ya Zanzibar, ambazo zinazungumzia uhuru wa watu kujieleza.

Aliongeza pia kwamba lazima sheria zikidhi vigezo vya kimataifa ili “kuiweka nchi yetu katika ramani ya kisasa ya uhuru wa habari”.

Aidha alisema kuwa Zanzibar kuna Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 8 ya mwaka 1997, na Sheria ya Tume ya Utangazaji ya mwaka 1997 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2010, lakini “kwa bahati mbaya zote zina changamoto nyingi ambazo zinahitaji marekebisho.”