Marubani waliozuia kutokea kwa ajali ya ndege nchini Tanzania kupewa tuzo Maalum

Wizara  ya Ujenzi na Uchukuzi nchini Tanzania, imesema  itawazawadia tuzo maalumu Rubani Suhad Soud Kassim na Ofisa Daraja la kwanza, Alessandro Morgan kutokana na ujasiri walioonesha na kufanikiwa kuzuia kutokea ajali ya ndege.

Marubani hao ni wa Shirika la Ndege (ATCL), imeeleza kuwa walionesha ujasiri kwa kuzuia kutokea ya ajali ya ndege yao yenye namba TC 110 Airbus  A 220 ikiwa na abiria 84.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gabriel Migire ameahidi hayo, wakati akifungua kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa  ATCL,lililofanyika Machi 30, 2022 mjini Morogoro 

“Wizara pia itafanya jambo kwa kutambua mchango mkubwa uliofanywa  na marubani hao , siyo kwa maana ya kupendelea na siyo kwa maana wengine hawakufanya vizuri, lakini  walifanya jambo la ajabu sana.Walifanya maamuzi magumu ambayo kwa kweli yanapaswa kutambuliwa na serikali na wadau wengine,” amesema Katibu Mkuu.

Kwa mujibu wa Uongozi wa  ATCL, marubani wa  ndege hiyo iliyokuwa  ikiruka jioni ya Septemba 29, 2020, Uwanja wa Kimataifa wa  Kilimanjaro ( KIA) kuelekea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, ikiwa kwenye kasi kujiandaa kuruka  marubani hao  walimuona mnyama kwenye njia ya kurukia.

Uongozi wa ATCL umeeleza kwamba marubani hao walitumia  ujasiri wa kuisimamisha ndege hiyo, ili isifikie  kumgonga mnyama huyo kwenye hatua ya kupaa angani, jambo lililoteta taharuki kubwa kwa abiria , ndugu na taasisi kwa ujumla.