Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka 746 likiwemo la kughushi na kutakatisha fedha haramu zaidi ya shilingi bilioni 4.7, mali ya benki ya NBC tawi la Mnazi Mmoja, Ilala, Dar es Salaam.
Washitakiwa hao ni Baraka Madafu, Mark Mposo, Lusekelo Mbwele, Leena Joseph, Bernard Mndolwa, Salvina Karugaba, Mohamed Kombo, Hussein Amani na Paul Shayo ambaye alienda kusomewa mashtaka katika hospitali ya Kitengule Tegeta alikolazwa.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Faraji Nguka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ritha Tarimo.
Ilidaiwa kuwa shitaka la kwanza linalowakabili washtakiwa wote ni kuongoza genge la uhalifu na kujipatia kiasi cha shilingi bilioni 4.7, kosa wanalodaiwa kulitenda kati ya Aprili 1, 2019 na Desemba 31, 2020 katika Benki ya NBC, tawi la Mnazi Mmoja, Ilala Dar es Salaam.
Katika shitaka la pili, wanadaiwa kuisababishia benki hiyo ya NBC, tawi la Mnazi Mmoja hasara huku shitaka la tatu likiwa ni utakatishaji fedha hizo zilizopatikana kwa njia haramu.
Nguka aliendelea kudai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa pia na mashtaka 371 ya kughushi nyaraka na mengine 371 ya kuwasilisha nyaraka za uongo, makosa ambayo waliyafanya katika tarehe hizo hizo na maeneo hayo.
Nguka alidai upelelezi wa kesi hiyo uko katika hatua za mwisho na wako katika mchakato wa kufungua jalada Mahakama Kuu ili kuendelea na hatua nyingine za kusikilizwa.
Hakimu Tarimo aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 13, 2022 na washtakiwa wote walipelekwa mahabusu kwa kuwa shtaka la utakatishaji fedha haramu halina dhamana.