Mbunge wa Kongwa ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kwa mara ya kwanza amehudhuria vikao vya Bunge leo Aprili 13, 2022 , tangu alipojiuzulu uspika Januari 6, mwaka huu.
Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, Spika Tulia Ackson, alisimama kwa ajili ya kutambulisa wageni, lakini kabla ya kufanya hivyo aliomba bunge kwa upekee atambue uwepo wa Ndugai.
“Naomba kabla ya kutambulisha wageni kwa upekee nitambue uwepo wa Spika mstaafu Job Ndugai,” amesema Spika wa Bunge Tulia Ackson na Bunge likalipuka kwa shangwe na makofi yaliyodumu kwa sekunde kadhaa…“Asanteni sana waheshimiwa wabunge kwa kumpa heshima hiyo Spika Mstaafu Job Ndugai.” Amesema Spika Tulia
Ndugai hakuwahi kuonekana katika shughuli yeyote rasmi ya Bunge, ikiwemo ziara na vikao vya kamati za bunge tangu ajiuzulu uspika.
Mara ya mwisho kuhudhuria vikao vya Bunge ilikuwa Novemba 12 mwaka jana akiwa Spika na ilikuwa ukomo wa Mkutano wa Tano wa Bunge la 12.
Hivyo Ndugai hakuhudhuria mkutano wa sita wa Bunge la 12 ambao ulifanyika kwa wiki tatu mwezi Februari mwaka huu na amekosa vikao vitano vya Mkutano wa saba ulioanza Aprili 5, 2022.
Hivi karibuni uongozi wa Bunge ulisema hauna taarifa rasmi ya udhuru ya Ndugai na Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema anachojua mbunge huyo yupo jimboni kwake.