Ripoti ya CAG yaonyesha dosari Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu 

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Tanzania CAG Charles Kichere, amebaini dosari katika mchakato wa utoaji wa fedha za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikiwa ni pamoja na kutopewa nafasi kwa vijana wanaotoka familia zenye kipato duni.

Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21 CAG Charles Kichere amesema alipitia orodha iliyotolewa ya wanafunzi walio chini ya uhitaji ili kuthibitisha kama mikopo inatolewa kulingana na mahitaji na kubaini kuwapo kwa dosari katika mgao wa waombaji 12,660.

CAG amefafanua kuwa alibaini waombaji waliopata mikopo chini ya uhitaji wao, waliopata mikopo lakini wakiwa na uhitaji hasi na waliopata mikopo mikubwa kuliko mahitaji yao.

“Pia, wakati nikichambua orodha ya wanafunzi waliopimwa uhitaji wa mkopo kwa mwaka wa masomo 2020/21, nilibaini wanafunzi 71 kutoka kaya maskini zenye kipato cha chini na walio katika Mpango Maalum wa Kusaidia Uchumi (TASAF) walidahiliwa katika vyuo vikuu mbalimbali lakini hawakupangiwa mikopo.

“Kutokukithi mahitaji kwa mchakato wa ugawaji wa mikopo kunachangiwa na ukweli kwamba uthibitishaji wa maombi hufanywa kabla ya mchakato wa ugawaji wa mikopo.

“Pia, kutowasilisha wanafunzi waliodahiliwa kwa wakati kunaweza kusababisha ugawaji mbaya wa mikopo kwa waombaji wenye uhitaji.

“Nina wasiwasi kuwa ucheleweshwaji wa udahili wa wanafunzi unaweza kusababisha kukosa mkopo kwa waombaji wanaostahili au kinyume chake. Pia, kunaweza kusababisha waombaji wanaostahili kukosa mikopo hiyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti,” anasema.

Katika mapendekezo yake, CAG anasema uongozi wa HESLB ufanye ukaguzi wa udhibiti wa mfumo wakati wa mchakato wa ugawaji wa mikopo na kuchukua hatua stahiki ili kufanya mchakato huo kuwa na ufanisi zaidi.

CAG pia anasema amebaini kutokuwapo taarifa za kutosha za mwajiri na wakopeshwaji kwa ajili ya ufuatiliaji wa mkopo, akifafanua kuwa wakati wa ukaguzi, alihoji kuhusu kuwapo kwa orodha ya waajiri na alipitia ili kuthibitisha usahihi na ukamilifu wa taarifa za waajiri kwa ajili ya ufuatiliaji mzuri wa wanufaika wa mikopo.

Anasema kuwa HESLB iliitoa orodha ya waajiri 6,840 lakini mapitio yalibaini kuwa orodha ya waajiri ina rekodi zisizo kamili na kwamba katika orodha hiyo, hakukuwa na namba ya mlipakodi kwa waajiri wote, waajiri 150 hawakuwa na anwani wala namba za simu.

“Zaidi, hakukuwa na kipengele cha taasisi kama ilivyobainishwa katika mwongozo kama vile balozi za Tanzania, balozi za nje, kamisheni kuu, kampuni, wamiliki wa biashara.

“Pia, nilipitia kanzidata ya wakopeshwaji katika mfumo wa LMS ili kubaini ukamilifu wa maelezo dhidi ya mahitaji ya mwongozo ambapo nilibaini kuwa baadhi ya taarifa zinazohitajika hazikuwa kamilifu. Taarifa hizo ni kama vile namba ya simu, barua pepe na anwani za mahali,” anasema.