Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Tanzania katika kipindi cha mwaka 2020/21, imebaini uwepo wa upungufu wa watumishi 8,356 katika mashirika ya umma 29.
CAG amebainisha kuwa kwa ujumla wanahitajika watumishi wapya 19,285.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kupitia ripoti hiyo, amesema katika ripoti ya mwaka 2019/20, ilibaini uwepo wa upungufu wa watumishi 4,092 katika mashirika na taasisi za umma 23 sawa na asilimia 37 ya idadi ya uhitaji.
Alibainisha kuwa mwaka huu tatizo hilo limeendelea katika taasisi 29 alizozikagua, na kubaini upungufu wa watumishi 8,356 sawa na asilimia 43 ya kiwango cha watumishi kilichopendekezwa cha watumishi 19,285.
Alitaja sababu za upungufu wa watumishi hao kuwa ni ucheleweshaji wa vibali vya kuajiri katika Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
“Hali hii inaleta athari mbaya kwa uwezo wa taasisi hizi kutoa huduma bora, ikiwa ni pamoja na kuelemewa na mzigo wa kazi na kushusha morali kwa watumishi waliopo, hivyo taasisi hizi zinaweza kushindwa kufikia malengo yake yaliyopangwa,” alieleza kupitia ripoti hiyo.
Alitaja taasisi hizo zenye upungufu wa watumishi kuwa ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linalohitaji watumishi takribani 4,741, Hospitali ya Taifa Muhimbili 4,567, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine 2,076, Mamlaka ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi 2,004 na Chuo Kikuu Mzumbe kinachohitaji watumishi 1,242.
Nyingine ni Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania 464, Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) 546, Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) 383, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) 739, Kampuni ya Stamigold 381, Makumbusho ya Taifa 165 na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) 133.
Pia Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere 349, Shirika la Usimamizi wa Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika 191, Taasisi ya Elimu Tanzania 255, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania 99, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi 85 na Bodi ya Kahawa Tanzania 104.
Aidha, zimo Bodi ya Usanifu wa Majenzi na Upimaji 75, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Lindi 72, Bodi ya Maziwa Tanzania 54, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) 126, Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania 28 na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) 48.
Pia, Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) 44, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro 19, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) 24, Taasisi ya Uhasibu Arusha 21, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga 60.
Kwa mujibu wa CAG, kwa sasa jumla wanahitaji watumishi katika mashirika hayo ya umma wapatao 19,285.
“Ninapendekeza Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iharakishe mchakato wa kutoa vibali vya kuajiri watumishi katika mashirika na taasisi zingine za umma,” alishauri.
Aidha, aliyataka mashirika ya umma yafuatilie katika Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhakikisha wanapata vibali vya ajira za kujaza nafasi za wafanyakazi wanaohitajika ili kutekeleza malengo ya taasisi hizo kwa ufanisi.