WHO,UNICEF YASEMA KUNA WASIWASI WA MLIPUKO WA UGONJWA WA SURUA

Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya surua huko kambini Beerta Muuri mjini Baidoa nchini Somalia.

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF na la afya duniani, WHO yamesema idadi ya wagonjwa wa surua duniani kwa miezi miwili ya mwanzo ya mwaka huu wa 2022 imeongezeka kwa asilimia 79 kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana na hivyo kuwa ni mazingira yanayoweza kuchochea mlipuko wa ugonjwa huo unaozulika kwa chanjo.

Taarifa ya UNICEF na WHO iliyotolewa jana jijini  New York, nchini Marekani na Geneva, Uswisi imesema, ongezeko la idadi ya wagonjwa wa surua kwa mwezi Januari na Februari mwaka huu ni dalili inayotia shaka juu ya hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo na inaweza kuchochea mlipuko mkubwa na kuathiri mamilioni ya watoto.

Mashirika hayo yamesema mvurugiko wa utoaji chanjo unaohusishwa na milipuko mingine ya magonjwa, ongezeko la ukosefu wa usawa katika kupata chanjo na kuelekezwa kwa rasilimali kutoka ratiba za chanjo za kawaida kunasababisha watoto wengine kusalia bila kinga dhidi ya surua na magonjwa mengine yanayozuilika.

Hatari ya mlipuko mkubwa zaidi inaongezeka kwenye jamii ambazo zimelegeza masharti ya kuepusha misongamano kwa ajili ya virusi vya Corona, hatua ambazo zilizingatiwa wakati janga la Corona lilipokuwa kubwa.

Zaidi ya hapo, watu wengi wakiwa wamefurushwa makwao kutokana ma mizozo na majanga kama vile Ukraine, Ethiopia, Somalia ,na Afghanistan, kuvurugika kwa ratiba za utoaji wa chanjo na janga la COVID-19,  ukosefu wa maji safi na salama, na mikusanyiko ya watu kupindukia, vinaongeza hatari ya mlipuko wa surua.

Taarifa hiyo imetaja nchi 5 ambako kuna idadi kubwa ya wagonjwa, ambapo orodha inaongozwa na Somalia, ikifuatiwa na Yemen, kisha Afghanistan, halafu Nigeria na ya tano Ethiopia.

UNICEF na WHO wanasema idadi ya wagonjwa inaongezeka pale utoaji chanjo unapopungua.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema, Surua ni ugonjwa  hatari na unaua. Hali ya sasa ni kiashiria cha pengo katika mpango wa kimataifa wa utoaji wa chanjo. Inatia moyo kuona watu wanajisia salama kurejea katika maisha ya kawaida baada ya kupata chanjo ya COVID-19. Lakini kufanya hiyo kwenye mazingira ambamo watoto hawapati chanjo za kawaida za kinga dhidi ya magonjwa ni kuweka mazingira sahihi ya kimbunga cha kuenea kwa magonjwa kama surua.

Mashirika hayo yamesema utoaji wa chanjo kwa asilimia 95 au zaidi, ukihusisha dozi mbili za chanjo dhidi ya surua, unaweza kulinda watoto dhidi ya surua.

Ni kwa mantiki hiyo UNICEF na WHO kwa ushirikiano na wadau wake wakiwemo GAVI na taasisi ya Bill na Melinda Gates wanaunga mkono uimarishaji wa mifumo ya utoaji chanjo kupitia hatua mbalimbali.

Miongoni mwa hatua hizo ni kurejesha huduma za kampeni za chanjo kwenye nchi ambako kuna mazingira ya kuwasilisha salama chanjo hizo. Pia kusaidia wahudumu wa afya na viongozi wa jamii kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo.