MCT, LHRC,: Katiba mpya isisubiri uchaguzi

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema Katiba mpya ni suala lenye utashi wa kisiasa hivyo mchakato wake unaweza kufanyika wakati wowote kwa kuwa ni hitaji la Watanzania wote...

0

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema Katiba mpya ni suala lenye utashi wa kisiasa hivyo mchakato wake unaweza kufanyika wakati wowote kwa kuwa ni hitaji la Watanzania wote na si vyama vya siasa pekee.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema hayo jana wakati akiwasilisha mapendekezo ya baraza hilo kwa kikosi kazi kilichoundwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ridhaa ya Rais Samia Suluhu Hassan ili kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu demokrasia, maridhiano, katiba mpya na mambo mengine.

Mukajanga alisema suala la katiba mpya lisigeuzwe kuwa ni utashi wa watu fulani wanaoshinikiza lifanyike.

“Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwa nafasi yake alishawahi kulianzisha na baadae likaishia pale lilipoishia. Ukiwepo utashi wa kisiasa linaweza kufanyika mwaka wowote,” alisema.

Alisema hata Rais John Magufuli alipoamua serikali ihamie Dodoma ni jambo aliloweza kulifanikisha kwa haraka ingawa suala hilo lilikuwa katika mijadala na mipango ya muda mrefu bila kutekelezwa.

Kuhusu hoja ya mikutano ya vyama vya siasa, alisema suala hilo kamwe halipaswi kuleta migogoro kwa kuwa lipo kwa mujibu wa katiba, hivyo kunapaswa kuwekwa utaratibu wa kuonesha kuna usawa kwa vyama vyote.

Hoja ya mawasiliano na uhusiano kwa umma na vyama vya siasa, Mukajanga alisema suala hilo halipaswi kuonesha urafiki baina ya vyama vya siasa na wanahabari kuwepo zaidi wakati wa Uchaguzi Mkuu pekee bali wakati wote.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Maboresho na Utetezi, Wakili Fulgence Massage alisema wanaona mchakato wa katiba mpya usiangalie uchaguzi unafanyika lini.

“Kuna haja ya kuwa na kamati ya wataalamu ili kuangalia maoni ya watu yanasemaje ila kimsingi tunaona kuwa suala hili halipaswi kusubiri hadi pale uchaguzi utakapopita,” alisema Massawe.

Awali Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema wanatarajia mchakato wa kukusanya maoni uwe umekamilika ifikapo Agosti mwaka huu na kukabidhi ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted