Serikali imeidhinisha ruzuku ya shilingi bilioni 100 ili kupunguza gharama za mafuta zilizotangazwa mapema mwezi huu huku ikiahidi hatua zaidi kupunguza bei za mafuta nchini.
Waziri wa Nishati, Januari Makamba amesema serikali inakamilisha taratibu za kupata mkopo kutoka katika Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB) ili kusaidia kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta katika soko la dunia.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya mafuta bungeni, waziri Makamba amesema, ruzuku hiyo haita athiri miradi ya serikali inayoendelea na uamuzi huo ni hatua ya serikali ya muda mfupi kupunguza ongezeko la bei ya mafuta kabla ya Mwaka mpya wa fedha.
Kauli ya Makamba imekuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu, kuelekeza serikali ijibane na ijinyime ili kupata fedha katika matumizi ya kawaida ya serikali zitakazoenda kutoa nafuu kwa wananchi katika bei ya mafuta kuanzia Juni Mosi mwaka huu.
Amesema katika mwaka ujao wa fedha serikali itachukua hatua za kikodi ili kuwapa wananchi ahueni ya bei ya mafuta.
Alhamisi iliyopita Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliitaka serikali leo ije na kauli kuhusu hatua za dharura za muda mfupi na za muda mrefu katika kukabili bei ya mafuta.
Waziri Makamba alisema mwezi Oktoba kodi mbali mbali zilipunguzwa ikiwemo tozo ya miundo mbinu ya bandari, tozo ya kuchakata inayolipwa kwa mamlaka ya forodha, tozo ya kupima na kuthibitisha mafuta inayolipwa kwa wakala wa vipimo, tozo ya kupima na kuthibitisha ubora iliyokuwa inalipwa na TBS, tozo inayolipwa kwa wakala wa meli, tozo kwa ajili ya kuthibitisha biashara ya mafuta EWURA na tozo ya huduma ya service levy.
“Kupunguzwa kwa kodi hizo zilizokuwa zinatozwa na taasisi mbalimbali kwenye mafuta, uamuzi huo ulisababisha mapato ya serikali yapungue kwa Sh bilioni 102.”Amesema Makamba
Amesema Machi mwaka huu bei ilipanda zaidi kwa pipa kuliko miaka 14 iliyopita ikafikia Dola za Marekani 137 ndio maana mwezi huu bei zimepanda na kufikia hali ilivyo sasa ambako kwa Dar es Salaam bei ya kikomo ya petroli ni Sh 3,148 kwa lita, dizeli ni Sh 3,258 na mafuta ya taa ni Sh 3,112 kwa lita
Aidha Makamba amesema bado nchi inaakiba ya kutosha ya mafuta na katika kila aina ya mafuta ina zaidi ya akiba ya siku 20