Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu nchini humo imesema imeendelea kufanya mapitio ya mitaala na miongozo ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuhakikisha mafunzo yanayotolewa katika ngazi hiyo yanaendana na mipango ya nchi na mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumza wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda amesema katika kufikia azma hiyo, Serikali kupitia Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, imehakiki mitaala 51 kati ya 150 iliyoandaliwa na vyuo vya elimu ya ufundi kwa lengo la kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira.
Amesema serikali imeandaa na kuhuisha mitaala 27 ya fani mbalimbali katika sekta tano ambazo ni umeme , magari, mitambo, kilimo na ukarimu.
Aidha, amesema mitaala 19 katika fani ya Biashara, Usafirishaji, Ujenzi na Mitambo ya Magari Moshi imeanza kuandaliwa.
“Imehuisha mihtasari nane kwa ajili ya masomo bebezi na mtambuka ambayo ni Stadi za Maisha, Ujasiriamali, TEHAMA, Sayansi ya Ufundi, Michoro ya Kiufundi, Lugha ya Kiingereza, Lugha ya Kifaransa na Biashara ya Utalii”– amesema Waziri Mkenda
Amesema wameandaa mwongozo wa mitaala ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na mwongozo wa kuwezesha wanafunzi kusajiliwa kusoma na kubadilishana watumishi katika vyuo vya ATC, NIT na DIT na imefanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mitaala na mihtasari iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili katika Vyuo 21 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs).
Hii leo wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa shilingi trilioni 1.493 ili kuiwezesha utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2022/23,
Akitoa mchanganuo wa fedha hizo Mkenda amesema Shilingi Billion 533.4 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya Wizara ambapo Shilingi Billion 500.19 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi Billion 33.26 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Amesema Shilingi Billion 54 zinaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo Shilingi Billion 778 ni fedha za ndani na Shilingi Billion 181.46 fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
“Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya UNESCO inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi Billion 2.7 kwa ajili ya matumizi ya kawaida (Mishahara ni Shilingi Billion.17 na matumizi mengineyo ni Shilingi Billion1 .5.”Amesema Mkenda