Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, nchini Tanzania Toba Nguvila ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama katika Wilaya hiyo kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaodaiwa kuchoma moto gari la Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nyamilanda wilayani humo, Emmanuel Sheiza nyumbani kwake.
Nguvila ametoa agizo hilo jana Mei 9, 2022 alipotembelea eneo la tukio na baadaye kuongea na wanakijiji wa kitongoji cha Nyamilanda na kuelezea masikitiko yake.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana ambapo watu wasiofahamika walichoma moto gari la Hakimu huyo ambaye anaishi kwenye nyumba za Mahakama zilizopo jirani na Mahakama ya Mwanzo Nyamilanda.
“Tayari tukio hili la kusikitisha limesharipotiwa katika vyombo vya ulinzi na usalama na uchunguzi unaendelea ili kuwakamata wahusika wote na hakuna hata mmoja atakayekwepa mkono wa chuma wa sheria” amesema Mkuu wa Wilaya huyo.