Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Burkina Faso imemuamuru Blaise Compaore kulipa fidia kutokana na mauaji ya Thomas Sankara - Mwanzo TV

Burkina Faso imemuamuru Blaise Compaore kulipa fidia kutokana na mauaji ya Thomas Sankara

Blaise Compaore, Rais wa zamani wa Burkina Faso

Mahakama nchini Burkina Faso Jumanne iliamuru aliyekuwa rais wa nchi hiyo Blaise Compaore na wengine tisa kulipa fidia ya zaidi ya dola milioni moja kwa jamaa za kiongozi wa mapinduzi Thomas Sankara na wasaidizi waliouawa mwaka 1987.

Amri hiyo inajiri baada ya kesi iliyoamuliwa mwezi uliopita na kuwahukumu waliohusika kwenda jela kwa muda mrefu, na kumaliza kesi iliyokumba nchi hiyo kwa miaka 34.

Rafiki wa zamani wa Sankara, Compaore alichukua mamlaka wakati wa mapinduzi yaliyofanyika kwenye siku ambapo Sankara pia aliuawa, Compaore alitawala hadi 2014 na kupinduliwa kwenye maandamano makubwa na kukimbilia nje ya nchi.

Jaji Urbain Meda, anayeongoza mahakama ya kijeshi katika mji mkuu wa Ouagadougou, aliamuru malipo ya franc za CFA milioni 807.5 ($1.3 milioni / euro milioni 1.2) kwa jamaa za watu 12 waliouawa kwa kupigwa risasi pamoja na Sankara.

Waliohusika na mauji ya Thomas Sankara ni Blaise Compaore, Hyacinthe Kafando, aliyekuwa kamanda wake wa walinzi wa rais; Gilbert Diendere, mkuu wa zamani wa jeshi mwaka 1987; na washtakiwa wengine saba.

Mnamo Aprili 6, Compaore, Kafando na Diendere walihukumiwa kifungo cha maisha kwa kupanga mauaji hayo, huku wengine wakifungwa miaka mitatu hadi 20 jela.

Compaore, ambaye anaishi katika nchi jirani ya Ivory Coast, alihukumiwa bila kuwepo wakati Kafando amekuwa mbioni tangu 2016. Chini ya uamuzi wa mahakama, serikali ya Burkina Faso inapaswa kuwafidia warithi wa waathiriwa ikiwa waliopatikana na hatia hawataweza kulipa.

Lakini mahakama ilikataa ombi la kurejesha mali ya Sankara kwa familia yake.

Benewende Stanislas Sankara, wakili wa Sankara, alionyesha majuto kwa uamuzi wa mahakama kuhusu kutorejeshewa mali ya Sankara kwa familia yake na kusema familia inazingatia kukata rufaa.

Sankara ambaye alikosoa nchi za Magharibi kwa ukoloni mamboleo na unafiki aliuawa kwa kupigwa risasi Oktoba 15, 1987, miaka minne tu baada ya kuingia madarakani kama nahodha wa jeshi akiwa na umri wa miaka 33 tu.

Yeye na wenzake 12 waliuawa na kikosi kilichoshiriki katika kikao cha Baraza la Mapinduzi la Taifa.

Kujadili kifo cha kiongozi huyo ilikuwa mwiko katika utawala wa miaka 27 wa Compaore.