Rais Umaro Sissoco Embalo alivunja bunge la Guinea-Bissau siku ya Jumatatu na kusema uchaguzi wa mapema wa bunge utafanyika mwaka huu ili kutatua mzozo wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu.
Mvutano kati ya bunge na urais umelikumba taifa hilo la Afrika Magharibi kwa miezi kadhaa.
Embalo alitaja tofauti zinazoendelea na zisizoweza kutatuliwa kwenye bunge ni siasa zisizo za haki na zimejaa njama nyingi.
“Mgogoro huu wa kisiasa umesambaratisha mtaji wa uaminifu kati ya taasisi huru,” alisema.
“Nimeamua kurudisha nafasi kwa Waguinea ili mwaka huu waweze kuchagua kwa uhuru bunge wanalotaka kuwa nalo.”
Amri ya rais ilisema uchaguzi wa bunge utafanyika Desemba 18.
Koloni la zamani la Ureno lenye takriban watu milioni mbili halijatulia na limekumbwa na mapinduzi manne ya kijeshi tangu 1974, mapinduzi ya hivi majuzi zaidi mwaka 2012.
Mwaka 2014, Guinea-Bissau iliapa kurejea katika demokrasia, lakini imekuwa na utulivu mdogo tangu wakati huo na majeshi yanashikilia nguvu kubwa.
Watu 11 walifariki mwezi Februari katika ghasia ambazo zilielezwa kuwa ni jaribio la mapinduzi.
Watu waliokuwa na silaha nzito walishambulia majengo ya serikali huko Bissau wakati rais alipokuwa akiongoza kikao cha baraza la mawaziri.
Embalo, ambaye amekuwa madarakani tangu 2019, baadaye aliwaambia waandishi wa habari kwamba alitoroka vita vya saa tano vya bunduki na kuelezea shambulio hilo kama njama ya kuiangamiza serikali.
Mnamo Februari 10, Embalo alisema mkuu wa zamani wa jeshi la wanamaji alikuwa miongoni mwa wanaume watatu waliokamatwa kutokana na shambulio hilo ambalo alilihusisha na biashara ya dawa za kulevya katika Bahari ya Atlantiki.
Guinea-Bissau ni kitovu cha usafirishaji wa kokeini kutoka Amerika Kusini hadi Afrika.
Wiki iliyopita, Embalo alimfuta kazi waziri wake wa uchumi na kukabidhi wizara yake kwa muda kwa waziri mkuu, amri ilisema.
Victor Mandiga aliondolewa ‘ili kuhakikisha utendakazi wa taasisi,” ilisema.
Waziri aliyefukuzwa hivi karibuni alipinga kile alichokitaja kama wizara ya fedha kuingilia baadhi ya masuala ya wizara yake, na wizara ya mambo ya nje kusimamia sekretarieti mpya ya serikali ya mtangamano wa kikanda ambayo ni majukumu ya wizara yake.
Kutoelewana kati ya Embalo, 49, na bunge kumejikita zaidi kwa kiongozi wa upinzani Domingos Simoes Pereira, ambaye alishindwa na Embalo katika uchaguzi wa rais uliokuwa na ushindani mkali mwaka 2019.
Bunge la Guinea-Bissau na rais pia wametofautiana kuhusu ugawaji wa rasilimali za mafuta kwenye mpaka na Senegal, marekebisho ya katiba na kutangazwa kwa kikosi cha kuleta utulivu kutoka kwa jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi ECOWAS.
Amri ya rais ya Jumatatu ilishutumu bunge kwa kuwalinda wabunge wanaoshukiwa kuhusika na ufisadi na kukataa kutii mashtaka dhidi yao.