Raia wawili kutoka nchini Kenya, wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha nchini Tanzania wakituhumiwa kuwa na magunia 15 ya mirungi.
Wakenya hao wanatuhumiwa kumiliki mirungi hiyo na kuisafirisha kwenda maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kukamatwa kwa wafanyabiashara hao na kusema bado uchunguzi wa tukio haujakamilika, lakini ukishakamkilika jalada litafikishwa kwa Mwanasheria wa Serikali kwa hatua nyingine za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamni.
Watuhumiwa hao walikamatwa maeneo ya Namanga, wakiwa katika gari ndogo aina ya Toyota Forester yenye namba za usajili KDC 922T, iliyokuwa ikiongoza gari kubwa, lililokuwa limebeba shehena hiyo Mei 14, 2022. Lakini baadaye gari hilo kubwa liliachiwa polisi, wakati mirungi ilishushwa kituoni hapo na gari ndogo pia inashikiliwa.