Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimeonya wanachama wa chama hicho wasiomheshimu Rais Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid Mohamed alitoa onyo hilo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa chama hicho, Dar es Salaam.
“Rais amefungua milango ya demokrasia nchini anapaswa kuungwa mkono na siyo kebehi na dhihaka, nani asiyejua kuwa vyama vya upinzani nchini vilikuwa kifungoni?. Leo hii Rais amefungua milango ya majadiliano nikiwa kama Makamu Mwenyekiti wa kikosikazi sipo tayari na ADC haipo tayari kuona Rais anakashifiwa kwa namna yeyote na kama kuna anayefikiria kufanya hivyo ndani ya ADC basi si mahala pake”alisema Hamad.
Alisema Rais Samia ametoa mwanga mpya katika demokrasia nchini hivyo anastahili kuungwa mkono badala ya kumkashifu.
Hamad alisema wanachama wa chama hicho wasiache kukikosoa kistaarabu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakapokosea na kwamba huo ndio uungwana.
Alimshauri Rais Samia awekeze zaidi katika elimu ili jitihada za kuvutia wawekezaji ziwe na manufaa zaidi.
“Nayasema haya leo hii kuwa Rais anajitahidi kuleta wawekezaji nchini lakini tusipowekeza katika elimu fursa zote zitachukuliwa na hao tunawaita watalii, kumbe watalii watakiwa wakija hapa nchini watukute siye tushaelimika hivyo tutagawana ujuzi na teknolojia na mambo haya yatafanikiwa endapo tutawekeza zaidi katika elimu” alisema Hamad.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ADC, Haji Shoka Hamisi alisema kuna haja ya kumpongeza Rais Samia kwa kukuza demokrasia nchini.
Hamisi alimpongeza Rais Samia kwa kutekeleza kwa vitendo kiapo chake cha kufanya kazi na yeyote mwenye uwezo wa kazi husika kwa manufaa ya nchi.
“Hilo tumeliona mara tu alipoapishwa na kisha kupanga safu ya wakuu wa mikoa akamteua Queen Sendiga kutoka chama hiki, huu ni udhihirisho kuwa anatembea katika kiapo chake haikuwa rahisi kwani hata wana CCM wenzake baadhi walimshangaa “alisema.