Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema changamoto ya kwanza aliyokutana nayo alipoingia madarakani ni kutoaminiwa kutokana na uwanamke wake.
Rais Samia ameyasema hayo jana akiwa Accra Ghana, katika meza ya majadiliano ya viongozi mbalimbali kitaifa wa Afrika, katika mkutano ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Itakumbukwa Rais Samia alishika kijiti cha uongozi nchini Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo hayati Dk.John Magufuli ambaye alifariki Machi 17,2021 katika hospitali ya Mzena iliyoko jijini Dar es salaam ambako alilazwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo.
Rais Samia amesema: “Changamoto ya kwanza niliyokumbana nayo ni watu wa Tanzania kutoniamini, walitilia shaka kama nilikuwa na sifa ya kuongoza, wakati nilipochukua hatamu kwa sababu ni mwanamke.
“ Wengine hawakuamini kuwa mwanamke anaweza kuwa Rais bora, hawakuamini kuwa naweza kuendesha nchi, lakini ndani ya mwaka mmoja nimewaonesha kuwa mwanamke anaweza na mwanamke hawezi kufeli,” amesema Rais Samia na kuongeza:
“Kwa mwaka mmoja nimeonesha nguvu ya mwanamke,” kauli ambayo imeonesha kuwakuna Marais wengine na kupiga makofi ya kumshangilia.
“Nimeendesha nchi kama alivyokuwa anaendesha mtangaulizi wangu na nimefanya mengi mazuri zaidi,” amesisitiza.
Rais Samia alichukua nafasi ya hayati Dk. John Magufuli aliyefariki Machi 17.
Amesema wakati anachukua madaraka kufuatia kifo cha mtangulizi wake, dunia ilikuwa ikikabiliwa na mlipuko mkubwa wa Covid 19, nchi nyingi ziliathirika kiuchumi, hata Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathirika, ambapo uchumi wake uliporomoka kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 4.7.
“Tunavyoongea hapa, katika kipindi changu cha mwaka mmoja uchumi umepanda na kufikia asilimia 5.2, matarajio yangu ni kufikia asilimia 6 mwaka 2025,” amesema.