Hukumu ya kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai nchini Tanzania Lengai Ole Sabaya na wenzake sita inatarajiwa kutolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha nchini humo.
Hukumu hiyo inatarajiwa kuamua hatima ya kiongozi huyo wa zamani na wenzake endapo wataachiwa huru, ama wataendelea kusalia kifungoni.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Julai,2021 ambapo imechukua takribani miezi saba hadi kufunga ushahidi kutoka pande zote mbili.
Hatima ya Sabaya inasubiriwa kwa hamu na watu wengi kufuatia umaarufu alioupata wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai,mkoani Kilimanjaro na hata baada ya kutenguliwa na kushtakiwa.
Sabaya alikamatwa Mei 27, mwaka jana jijini Dar es salaam katika wilaya ya Kinondoni na kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Juni 4, 2021 na kufunguliwa kesi mbili tofauti ambazo ni ya Uhujumu Uchumi na ya Wizi wa kutumia silaha.
Katika kesi ya kwanza walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, hukumu ambayo Mei 6, 2022 ilitenguliwa na Mahakama Kuu baada ya kushinda rufaa waliyokata kupinga hukumu hiyo na kuwaachia huru baada ya kubaini dosari zilizojitokeza katika mwenendo wa kesi ya msingi katika mahakama ya chini.
Rufaa hiyo ilikatwa na Sabaya na wenzake wawili, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, wakipinga hukumu ya kifungo iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Jaji Sedekia Kisanya wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma aliyekuwa akisikiliza rufaa iliyokatwa na Sabaya na wenzake, alisema mahakama inabatilisha mwenendo wa kesi ya msingi na kutengua hatia dhidi ya warufani hao na adhabu iliyotolewa dhidi yao inatupiliwa mbali.
Katika kesi ya uhujumu uchumi inayotarajiwa kutolewa hukumu leo, mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021, Jamhuri ilikuwa na mashahidi 13 huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi nane.
Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na jopo la mawakili watano huku mmoja wa washtakiwa, Mwahomange akijitetea mwenyewe.
Machi 31 mwaka huu Hakimu Mkazi Mwandamizi Patricia Kisinda aliyekuwa akisikiliza shauri hilo la jinai, alisema atatoa hukumu hiyo leo baada ya pande zote kuwasilisha hoja zao za majumuisho.