Tanzania yajipanga kuweka mfumo wa Mtuhumiwa kujidhamini mwenyewe

Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Dk. Damas Ndumbaro, amesema wizara yake inakwenda kuufumua mfumo wa jinai, ili kuangalia namna ya kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani. 

Dk. Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu maswali ya wabunge, Elibariki Kingu (Singida Magharibi) na Felista Njau (Mbunge Viti Maalum), ambao waliohoji mkakati wa Serikali katika kutatua changamoto ya mrundikano wa mahabusu gerezani.

Waziri huyo, amesema marekebisho ya mfumo huo yatafanyika katika mwaka wa fedha ujao wa 2022/23, ambapo pamoja na mambo mengine, wizara hiyo itaangalia utaratibu wa kuanzisha adhabu mbadala ili kupunguza msongamano huo.

“Wakati tunapitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria mwaka huu, tulisema moja kati ya vipaumbele ni kwenda kuangalia, kuufumua na kuupanga upya mfumo wa jinai hapa nchini. Katika mpango huo moja kati ya jambo ni hili, kuangalia adhabu mbadala ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu katika magereza,” amesema Dk. Ndumbaro.

Aidha, Dk. Ndumbaro, amesema Serikali itaangalia uwezekano wa kuanzisha utaratibu wa watuhumiwa kujidhamini wenyewe, endapo zoezi la upangaji anuani za makazi na utoaji vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), litakapokamilika.

“Lengo la mtuhumiwa kujidhamini au kudhaminiana ni kuhakikisha anarudi mahakamani kwa tarehe atakayotakiwa. Kwa hivi sasa Serikali imejikita katika mpango wa kuweka anuani za makazi, pindi zoezi hili litakapokamilika tutakuwa na uwezo wa kujua kila mtu anaishi wapi,” amesema Dk. Ndumbaro na kuongeza:

“Hivyo, kutakuwa na uwezekano wa kujidhamini wenyewe. Kazi hii ikikamilika pamoja na vitambulisho vya taifa itawezesha Watanzania kujidhamini wenyewe, hivyo kupunguza msongamano wa mahabusu ambao watakuwa wako nje.”

Awali, Kingu aliihoji Serikali kama haioni umuhimu wa kuanzisha sheria itakayowezesha watuhumiwa kujidhamini wenyewe ili kupunguza mzigo wa mahabusu.

“Kwa kuwa idadi kubwa ya mahabusu walioko nje kwenye magereza wanaipa mzigo mkubwa Serikali yetu wa kuwahudumia. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta sheria itakayowezesha watuhumiwa wakapewa nafasi ya kujidhamini wenyewe, ili kupunguza mzigo na kuwapunguzia adhabu wananchi wanaoteseka magerezani kwa makosa ambayo yanaweza kudhaminika?” amesema Kingu.

Naye Njau alihoji “kwa kuwa kero kubwa ya msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani imekithiri. Je, Serikali inaonaje ikaleta utaratibu wa vifungo vya nje kwa makosa madogo madogo ili kupunguza msongamano huo?”

Tanzania bado inakabiliwa na msongamano mkubwa wa mahabusu katika magereza mbalimbali, ambapo wadau wa haki za binadamu na masuala ya sheria wakionya kwamba kuna haja sasa kwa serikali kubadilisha mifumo ili kukabiliana na hali hiyo.