Mtu mmoja anayeaminika kuwa raia wa Burundi ameuawa na wananchi kwa tuhuma za kujaribu kufanya tukio la uporaji kwa kutumia bunduki ambapo pamoja na kifo hicho bunduki moja aina ya AKA 47 imekamatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, James Manyama aliwaambia waandishi wa habari mjini Kigoma kuwa mtu huyo ambaye jina lake halijafahamika, alitaka kufanya uhalifu huo juzi jioni katika Kijiji cha Kibuye Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Awali kabla ya kutekeleza azma yake hiyo, akiwa amejificha kwenye kichaka alikutana na mwananchi wa kijiji hicho, Yapemacho Kasiano ambaye alimhoji mtu huyo sababu ya kujificha kichakani na alijibu kuwa alikuwa anatafuta njia ya kwenda Burundi.
Alisema wakiwa kwenye majadiliano hayo, ndipo mtu huyo alitoa bunduki aliyokuwa ameficha kwenye koti lake na kumshambulia mwananchi huyo. Hata hivyo, risasi ilimkosa na ndipo akamrukia mtu huyo na kuanza kupigana akitaka kumnyang’anya bunduki huku akipiga kelele.
Kutokana na kelele hizo, wananchi walijitokeza kwa wingi na kuanza kumshambulia kwa silaha mbalimbali za jadi ikiwamo mikuki na mapanga. Alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali baada ya kuvuja damu nyingi.
Kamanda Manyama alisema polisi walikamata bunduki moja aina ya AKA 47, risasi nne na ganda moja la risasi ambayo imetumika.
Akitoa mwendelezo wa taarifa ya watu waliokamatwa na viungo vya binadamu Juni 3 mwaka huu, Kamanda Manyama alisema polisi wamefukua kaburi la mtu ambaye viungo hivyo vilifukuliwa na kuthibitisha kuwa vilikuwa ni viungo vya Bilihanyuma Suminda (90) ambaye alizikwa Januari mwaka huu.
Aliwataja watuhumiwa ni Bankana Zakayo (41) aliyekuwa Sengerema Mkoa wa Mwanza ambaye alikuwa akipelekewa viungo hivyo.
Mwingine ni Miraji Nyambi (45) aliyekuwa dereva wa gari lililokamatwa na viungo hivyo ambao wote ni walimu wa Shule ya Sekondari Mwandiga Wilaya ya Kigoma.
Aliwataja watuhumiwa wengine ni Mathayo Ndayishimiye (40) mganga wa kienyeji kutoka Burundi, Ramadhani Abdulrahman (52), mganga wa kienyeji, Adizino John (62), Nguno Manyanza (49), James Kibeba (68), Kelvin Fedha na Thobias Fundo (33).